Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limetoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tukio la kupotea kwa wasichana wawili, Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu ‘Rahma’ (22), kuzifikisha polisi ili kusaidia kufanikisha uchunguzi huo.

Wasichana hao wanadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Juni 20, 2025 mkoani Arusha, baada ya kuhudhuria sherehe ya kupongezana kwa kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza chuoni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.

“Tunaendelea na upelelezi ikiwa ni pamoja na kuwahoji watu mbalimbali kuhusiana na tukio la kupotea kwa wasichana hao.

“Pamoja na taarifa mbalimbali ambazo zimeshakusanywa, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yoyote mwenye taarifa ambazo zinaweza kusaidia kufanikisha uchunguzi huu, asisite kuzifikisha kwani zitapokelewa na kufanyiwa kazi kwa haraka kusaidia kazi ya upelelezi wa tukio hilo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha miongoni mwa watu waliohojiwa ni wazazi wa Kareen wakazi wa kahama Mkoani Shinyanga.

Dada wa Kareen, Elizabeth Didas amesema kuwa maofisa wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga wamefika nyumbani kwao Kahama na kuchukua maelezo ya wazazi wa Kareen.

“Walifika walitaka kujua baadhi ya taarifa hasa mara ya mwisho kuongea na ndugu yetu, lakini shughuli zake na mambo mengine ya kifamilia,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Migomi alipoulizwa juu ya taarifa hizo amesema kuwa taarifa sahihi zichukuliwe kwa Polisi Arusha.

“Sehemu sahihi ya kupata taarifa za tukio hilo ni huko huko Arusha, naomba wasiliana na kamanda wa Polisi katika Mkoa huo,” amesema.

Awali, Mfanyabiashara Godwin Ndossi mkazi wa Shangarai mkoani Arusha anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano juu ya tukio hilo.

Wakili wa Ndossi, Liberia Mosoi amesema kuwa mteja wake alikwenda kujisalimisha katika kituo cha Polisi cha kati na baada ya maelezo aliendelea kushikiliwa.

“Mteja wangu alifika Polisi kutoa maelezo baada ya kuona anatuhumiwa mitandaoni, na baada ya kuchukuliwa maelezo ametakiwa kubaki kwa taratibu zingine za kipolisi,” amesema.

Awali tukio lilivyokuwa

Awali, taarifa za kupotea kwa wasichana hao ilianza kusambaa mitandaoni Mei 2, 2026 huku mfanyabiashara huyo akituhumiwa kuwaita katika sherehe ya usiku.

Wasichana hao wawili, Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu kama ‘Rahma’ (22), wanadaiwa kuhudhuria sherehe hiyo  Juni 20, 2025 eneo la shangarai wilayani Arumeru na tangu siku hiyo hawajaonekana hadi sasa.

Hata hivyo, tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Tengeru na kupewa jalada namba TEG/RB/342/2025.

Kareen alikuwa akiishi eneo la Shangarai, wilayani Arumeru, akijishughulisha na biashara ndogo ndogo pamoja na masomo ya uhasibu katika Chuo Kikuu Huria.

Kwa upande wa Nakivona, alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha akimalizia mwaka wake wa kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *