
Manchester, England. Jezi zitakazotumika na Manchester United katika msimu ujao, zimewekwa hadharani huku klabu hiyo ikipanga kuanza kuzivaa katika mechi zake mbili za mwisho za Ligi Kuu England msimu huu.
Uamuzi huo ni muendelezo ambao umeanza kuwa maarufu katika misimu ya hivi karibuni wa klabu za Ulya kutambulisha jezi za msimu unaofuata na kuanza kuzitumia kabla ya msimu huo haujaanza ili kushawishi idadi kubwa ya mashabiki kununua katika mapumziko ya msimu kipindi cha dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Jezi hizo za Man United zitakazotumika katika msimu wa 2026/2027, zimetengenezwa na kampuni ya Adidas na zimebuniwa kwa kuendana na jezi za timu hiyo zilizotumika miaka ya 1970.
Jezi hizo zitakuwa na kola isiyo ya duara ambayo itakuwa na neno ‘United’ katika mzunguko wa kola hiyo.
Mechi ambazo Man United itazitumia jezi hizo ni dhidi ya Nottingham Forest na Brighton.
Man United inafuata nyayo za Arsenal ambayo ilifanya jambo kama hilo mwaka jana katika mechi dhidi ya Newcastle United.
Pia Tottenham Hotspur imefanya hivyo ambapo imeshatambulisha jezi zake za msimu ujao ambazo zinasadifu toleo la 1987 walilotumia katika Fainali ya Kombe la FA.
Jana usiku, Bayern Munich nao walitambulisha jezi zao za msimu ujao walipozivaa katika mechi yao ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG.
Tayari jezi hizo za msimu ujao za Man United zimeshaingizwa sokoni na zinatarajiwa kuteka biashara kutokana na kitendo cha timu hiyo kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.