
Dodoma. Muswada wa kubadili sheria ya kuwezesha vyeti vya kitaaluma kutambuliwa kwa ajili ya mikopo uko mbioni kutua bungeni, lengo ni kuwezesha vijana wasomi kupata mikopo.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Mei 7, 2026 na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ambaye amesema inashangaza kuona kipande cha ardhi chenye thamani ya Sh15 milioni kinamwezesha mtu kupata mkopo benki wakati cheti cha mtu aliyesoma kwa zaidi ya Sh200 milioni hakitambuliki.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu kueleza mpango huo, kwani alishasema jambo hilo litafanyika na leo ametangaza muswada uko mbioni kutua Bungeni.
“Hapa tunaona kuwa tunabana wigo kwa vijana wetu kutokana na masharti haya, muswaada uko mbioni ili kuwafanya vijana waweze kudhaminika mpango huo ni kubadili sheria ili kutoka dhamana zisizohamishika na kurudi kwenye dhamana zinazohamishika,” amesema Dk Mwigulu.
Katika swali la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mbunge wa Kyerwa (CCM), Khalid Nsekela amemuuliza Waziri Mkuu Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wanaomaliza vyuo vikuu ambao wanakosa ajira kwa sababu ya kukosa ujuzi wataandaliwa ili wasiwe wanasumbuka kwenye ajira.
Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshasaini makubaliano kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuwa washindani kwenye masuala ya ajira.
“Lakini Mheshimiwa Spika, ni juzi tumepokea andiko kupitia kwa Mbunge Dk Selemani Jafo (Mbunge wa Kisarawe) kuhusu namna ya kuwawezesha vijana wasomi wasiokuwa na ajira,” amesema Dk Mwigulu.
Amesema Serikali kupitia taasisi zake wataendelea kutazama fursa za umma na sekta binafsi ikiwemo kuangalia uwezekano wa kuwa na dirisha la wahitimu ili vijana wenye mawazo ya ubunifu waweze kusaidiwa.
Katika mchango wake kwa Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora, alieleza nia yake ya kupeleka andiko Serikali la jinsi ya kuwezesha kuwa na ajira ya muda kwa wahitimu kabla ya kupatiwa au kuingia katika ajira rasmi.
Pendekezo la Dk Jafo, lilieleza namna inavyowezekana na jinsi ilivyo rahisi kutoa ajira hizo na kuwalipa vijana kwenye ajira za muda huku akieleza kuwa wengi wana ujuzi lakini wapo mitaani hivyo wakipatiwa ajira hizowanaweza kuziba pengo hilo.