Dar es Salaam. Siku chache baada ya kutangaza faida ya Sh206 bilioni iliyoipata katika robo ya kwanza ya mwaka huu, na hivyo kuifanya kuwa taasisi kubwa zaidi ya fedha nchini na inayoongoza kwa faida kubwa, Benki ya CRDB imewahakikishia wawekezaji wake uendelevu wa mwenendo huo.

Hakikisho hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, kwenye kongamano la wawekezaji na wadau lililofanyika jijini Dar es Salaam likiwa na kaulimbiu ya “Dira ya Pamoja ya Ukuaji”, likiwakutanisha wawekezaji, mamlaka za usimamizi, taasisi za umma na binafsi pamoja na washirika wa kimkakati kuelekea Mkutano Mkuu wa Wanahisa (AGM) utakaofanyika wiki ijayo.

Dk Nsekela amesema mafanikio yaliyopatikana yanaakisi utekelezaji madhubuti wa mkakati wa muda wa kati wa biashara, imani kubwa ya wateja, uwekezaji katika mageuzi ya kidijitali pamoja na upanuzi endelevu wa shughuli zake kikanda.

“Tukiwa na zaidi ya mawakala 40,000 wa CRDB, ATM zaidi ya 700 pamoja na matawi zaidi ya 260, benki inaendelea kukuza ujumuishi wa kifedha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa mamilioni ya watu tunaowahudumia,” alisema Dk Nsekela.

Licha ya faida hiyo nono, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 18.9 ikilinganishwa na ile iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka jana, Dk Nsekela amesema jumla ya mali za benki imefikia Sh23.9 trilioni, amana za wateja zimefikia Sh16.2 trilioni huku mikopo na dhamana ikiongezeka kufikia Sh14.7 trilioni.

Amesema CRDB imeendelea kuongoza soko kwa kuhifadhi asilimia 28 ya amana za wateja, asilimia 27 ya thamani ya mali, asilimia 29 ya mikopo na dhamana zote zilizotolewa na taasisi za fedha nchini, pamoja na kupata asilimia 30 ya faida baada ya kodi miongoni mwa zaidi ya benki 40 zilizopo nchini.

Ukuaji huu wa benki unachochewa na uwekezaji mkubwa katika mageuzi ya kidijitali yanayobadilisha upatikanaji wa huduma za fedha nchini na duniani kwa ujumla.

Amesema asilimia 98 ya miamala yote sasa inafanyika nje ya matawi huku asilimia 50 ya akaunti mpya zikifunguliwa kupitia majukwaa ya kidijitali na asilimia 40 ya miamala ikifanyika nje ya muda rasmi wa kazi wa matawi.

Kuhusu uwezeshaji biashara, amesema benki imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh2.1 trilioni kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, iliyowanufaisha zaidi ya wajasiriamali 120,000 huku zaidi ya Sh302 bilioni zikiwafikia wafanyabiashara wadogo 110,000.

Dk Nsekela amesema uwepo wa CRDB katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na Dubai umeendelea kuimarisha biashara za kikanda na kuunganisha wafanyabiashara na fursa mpya za masoko barani Afrika, Ghuba ya Uarabuni pamoja na Asia.

Akizungumzia thamani inayozalishwa kwa wanahisa, Dk Nsekela amesema CRDB ilizalisha thamani ya zaidi ya Sh1.72 trilioni mwaka 2025 kupitia kodi, gawio, mishahara, upanuzi wa biashara pamoja na kusaidia wadau mbalimbali.

Aidha, alisema benki hiyo inaendelea kuwa miongoni mwa kampuni kubwa zaidi zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ikiwa na thamani ya soko inayozidi dola za Marekani bilioni 2.8 huku bei ya hisa ya benki ikiongezeka kwa asilimia 253 kati ya Desemba 2023 na Aprili 2026.

Wakati huohuo, kampuni tanzu za CRDB zimeendelea kukua na kuimarika kiutendaji katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 ambapo CRDB Bank Burundi ilipata faida baada ya kodi ya Sh12.9 bilioni, CRDB Bank DR Congo faida ya Sh828 milioni huku CRDB Insurance ikipata faida ya Sh1.8 bilioni. Kwa upande wake, CRDB Bank Foundation imeendelea kukuza ujumuishi wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na vijana, ikiwafikia zaidi ya wanufaika 949,000 katika ukanda mzima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, amesema mafanikio hayo yanaonyesha utekelezaji wenye nidhamu, usimamizi bora pamoja na maono ya muda mrefu yaliyo wazi.

“Kaulimbiu ya kongamano la leo, ‘Dira ya Pamoja ya Ukuaji’, inaakisi imani yetu kuwa ukuaji endelevu lazima uzalishe thamani kwa wadau wote; wateja wetu, wawekezaji wetu, wafanyakazi wetu pamoja na uchumi tunaouhudumia.

“Kama Bodi, tunaendelea kujizatiti kuhakikisha ukuaji huu unaendelea kuwa endelevu, unasimamiwa vizuri na unaendana na maslahi ya muda mrefu ya wadau wetu wote,” amesema Profesa Mori.

Ameongeza kuwa Bodi imeendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora, usimamizi wa vihatarishi pamoja na ulinganifu wa kimkakati ili kuhakikisha benki inaendelea kuwa imara, yenye ushindani na tayari kwa mustakabali katika mazingira ya kifedha yanayoendelea kubadilika.

Kongamano hilo pia lilihusisha wasilisho maalumu kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) lililotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara na Uendelevu wa DSE, Innocent Mbele, kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa DSE, ambapo aliangazia mchango unaozidi kuongezeka wa masoko ya mitaji katika kuchochea upatikanaji wa fedha za muda mrefu, kusaidia ukuaji wa taasisi pamoja na kuharakisha mageuzi mapana ya uchumi wa Tanzania.

Ametumia fursa hiyo kuipongeza CRDB kwa utendaji wake imara pamoja na kuendelea kuongoza katika masoko ya mitaji, akibainisha kuwa ukuaji endelevu wa benki, ongezeko la thamani kwa wanahisa pamoja na imani kubwa ya wawekezaji vinaendelea kuiweka benki hiyo miongoni mwa taasisi bora zaidi zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *