
Kibaha. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka wawekezaji katika sekta ya mafuta kutumia fursa ya ujenzi wa barabara nane na zile za kulipia zinazotarajiwa kujengwa barabara ya Morogoro kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujazia mafuta na gesi.
Kunenge ametoa wito huo leo Alhamisi Mei 8, 2026 alipokuwa akizindua kituo cha kwanza cha kujaza mafuta kinachomilikiwa na kampuni ya GSM, kilichopo Kibaha Picha Ya Ndege mkoani humo.
Amesema kukamilika kwa barabara hizo si tu zitasaidia kukuza biashara katika mkoa huo bali kutaongeza pia uhitaji wa huduma za mafuta na gesi katika vyombo vya moto na kuwataka wawekezaji kuichangamkia fursa hiyo.
“Kama mlivyosikia serikali inajenga barabara nane zitakazoenda hadi Chalinze lakini pia kutakuwa na barabara za haraka ambazo watu watazilipia, zote hizi ni fursa kwenu kuweka vituo katika mkoa huu kwa kuwa biashara itakuwepo na hamtajutia,”amesema Kungenge.
Kunenge amesema magari 28,000 hupita kila siku katika Mkoa huo kwa barabara ya Morigoro na robo tatu yake ni magari makubwa huku asilimia iliyobaki ikiwa ni magari madogo na vyombo vingine vya moto.
Pia, amesema tayari mkoa huo una bandari kavu ya Kwala ambapo wanatarajia asilimia 70 ya mizigo inayoingia na kutoka bandatini itaenda huko na hivyo biashara kwa mkoa wa Pwani itazidi kukua.
Jingine ameeleza kuwa kuna ukuaji mkubwa wa viwanda, ambapo kabla ya kabla ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kulikuwa na viwanda 1688 lakini kwa sasa vimeongezeka na kufika 1722, kati ya hivyo vikubwa na vya kati ni 457 ambapo kumekuwa na ongezeko la viwanda 269.
“Kwa hiyo mnaweza kuona ukubwa wa uwekezaji na ukubwa wa biashara ulipo katika mkoa wetu ambao wote unahitaji huduma zenu pia..
“Pia ombi langu jingine ambalo najua uwezo mnao wa kulifanya hilo ni kuanzisha kwa vituo vya kujazia gesi sababu utumiaji wa vyombo vya moto kutumia gesi umeshaanza,”amesema Kunenge.
Ili kutekeleza hilo aliwashauri GSM na wadau wengine wa vituo vya mafuta kuwasiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) kuona ni maeneo gani ambayo yatahitaji kuwekwa huduma kama hizo ili waweze kuanza mipango ya kuwekeza kwa kuwa kama ni michoro ipo tayari .
Kuhusu kituo kilichozinduliwa, Kunenge amesema amefurahishwa na
ubunifu katika ujenzi wake kwa kuwa mbali na eneo la kujazia mafuta pia kuna huduma mbalimbali zinazopatikana hapo ikiwemo eneo la kutengeneza na kuoshea magari pamoja na mgahawa.
“Kubwa lililonifaraji zaidi ni kuwa uwekezaji katika maeneo hayo mengine mtayakodisha kwa watu wengine na hivyo kuleta maana ya kuishirikisha jamiibinayowazunguka katika uwekezaji huu,”amesema.
Awali akitoa taarifa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GSM Tanzania, Yassir Nassoro, amesema kituo hicho cha Kibaha ni cha kwanza kati ya vituo vitatu vya mafuta vitakavyoendeshwa na GSM Energies.
Nassoro amesema kituo kingine kinatarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni eneo a Mbagala jijini Dar es Salaam, kikifuatiwa na kituo cha Tunduma karibu na mpaka wa Zambia kwa lengo la kuhudumia kwa ufanisi ukanda huo muhimu wa usafirishaji na biashara.
“Ukiacha vituo vya mafuta, GSM Energies pia ina kitengo kinachojihusisha na uhifadhi pamoja na usafirishaji wa petroli na dizeli katika ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika Kati na Kusini mwa Afrika ikiwa na zaidi ya malori 300 na kutilo ajira zaidi ya 300 hadinsasa,”ameaema Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo Nassoro alitoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji wa sekta binafsi, ubunifu na ukuaji wa uchumi nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,Nickson Simon, amesema wanajivunia Kibaha kuwa eneo la kwanza kwa GSM kuweka kituo chao cha mafuta.
Simon amesema uwekezaji huo kwao una maana kubwa sio tu kuwepo kwa kituo bali inamaanisha kufungua huduma, kuleta maendeleo ya mji huo na kuongeza ukusanyaji wa kodi kwa serikali.