Arusha. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Arusha umeanza zoezi la kuondoa shughuli za kibinadamu, ikiwemo biashara na miundombinu ya maji na umeme, iliyopo ndani ya hifadhi ya barabara ya Arusha Bypass, katika juhudi za kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara katika eneo hilo.

Hatua hiyo inafanyika sambamba na maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa pamoja na maboresho ya miundombinu kuelekea Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Akizungumza leo Jumamosi Mei 9, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Christopher Sauli, amesema utafiti umebaini ongezeko la shughuli za kibinadamu kandokando ya barabara hiyo limechangia kwa kiasi kikubwa ajali.

Amesema uwepo wa vibanda, biashara za mchanga na matofali pamoja na msongamano wa watu umekuwa ukiweka hatarini watumiaji wa barabara hiyo.

“Tumeona wazi kuwa shughuli hizi ndani ya hifadhi ya barabara zimekuwa chanzo cha ajali. Tumeanza kuondoa vibanda na miundombinu yote iliyopo ndani ya eneo hilo ili kuongeza usalama,” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na biashara, miundombinu ya maji na umeme pia itaondolewa ndani ya hifadhi ya barabara ili kuweka mazingira salama kwa watumiaji.

Kuhusu mradi wa barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa, amesema tayari mkandarasi amekabidhiwa eneo la kazi na ameanza maandalizi, huku TANROADS ikihakikisha eneo la mradi linakuwa huru kabla ya ujenzi kuanza.

Amesema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake, zinazokataza shughuli zozote kufanyika ndani ya hifadhi ya barabara bila kibali.

Kwa upande wake, baadhi ya wananchi wa Mbauda wameunga mkono hatua hiyo wakisema itasaidia kupunguza ajali na kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara, licha ya kuwepo kwa changamoto kwa wafanyabiashara waliokuwa wakitegemea maeneo hayo.

Tanroads imetoa wito kwa wananchi kuondoa shughuli zao kwa hiari ndani ya hifadhi ya barabara ili kuepuka usumbufu na kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *