
Singapore. Serikali ya Singapore imethibitisha kuwa walimu katika shule za nchi hiyo wana ruhusa kutumia viboko kama adhabu kwa wanafunzi wenye utovu mkubwa wa nidhamu, hatua ambayo imeendelea kuzua mjadala kuhusu athari zake kwa afya ya akili ya watoto.
Waziri wa Elimu wa Singapore, Desmond Lee amesema viboko vinaendelea kutumika kama hatua ya mwisho pale mbinu nyingine za nidhamu zinaposhindwa kusaidia.
“Shule zetu hutumia viboko kama hatua ya kinidhamu iwapo njia nyingine zote hazitoshi kutokana na uzito wa kosa lililofanywa,” amesema bungeni wakati akijibu maswali kuhusu hatua mpya za kupambana na unyanyasaji shuleni.
Hili linakuja katika kipindi ambacho katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Tanzania, kumekuwa na mijadala ya kutokomeza adhabu hiyo kwa kile kinachoelezwa kuwa huishia kuwaumiza watoto na si kuwafunza.
Akitoa ufafanuzi wa hilo, Lee amesema viboko hivyo hutolewa chini ya taratibu maalumu ili kuhakikisha usalama wa mwanafunzi unazingatiwa.
Amesema adhabu hiyo lazima iidhinishwe na mkuu wa shule na kutekelezwa na walimu waliopatiwa mamlaka maalumu pekee.
“Shule huangalia mambo mbalimbali, ikiwemo umri na ukomavu wa mwanafunzi pamoja na kama adhabu hiyo itamsaidia kujifunza kutokana na kosa lake,” amesema Lee.
Hatua hiyo ni sehemu ya mfumo mpya wa kupambana na vitendo vya uonevu mashuleni unaotarajiwa kuanza kutumika rasmi katika shule za Singapore kuanzia mwaka 2027.
Kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Elimu ya Singapore, viboko hutumika kwa wavulana pekee na kwa makosa makubwa kama suluhisho la mwisho.
“Viboko ni chaguo la kinidhamu kwa wavulana tu na hutumika kwa makosa makubwa pale inapokuwa lazima kabisa,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo.
Waziri Lee amesema mfumo huo unatokana na tafiti zinazoonyesha kuwa watoto hujifunza kufanya maamuzi bora wanapowekewa mipaka yenye adhabu zenye maana.
Hata hivyo, hatua hiyo imeendelea kuzua mjadala duniani kuhusu athari za adhabu za viboko kwa afya ya akili ya watoto.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likipinga matumizi ya adhabu za viboko kwa watoto, likisema zinaweza kuathiri afya ya mwili na akili kwa muda mrefu.
Katika ripoti yake ya mwaka 2025, WHO ilisema ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa adhabu za viboko zina madhara mengi kwa watoto bila kuwa na faida za moja kwa moja kwa jamii au familia.
“Matokeo ya adhabu za viboko yanaweza kudumu maisha yote na kuathiri afya ya akili, elimu pamoja na maendeleo ya kijamii ya mtoto,” ilieleza ripoti hiyo.
Singapore inafahamika duniani kwa sheria zake kali na utekelezaji mkali wa nidhamu kwa wananchi na wageni.
Mwishoni mwa Aprili mwaka huu, mtoto mmoja kutoka Ufaransa alishtakiwa nchini humo kwa kosa la kurudisha mrija wa kunywea juisi kwenye mashine ya vinywaji baada ya kuuramba, kosa ambalo linaweza kumfanya afungwe hadi miaka miwili gerezani.
Moja ya kesi zilizowahi kuvuta mjadala mkubwa duniani ni ile ya mtoto raia wa Marekani, Michael Fay aliyepigwa viboko mwaka 1994 baada ya kutiwa hatiani kwa uharibifu wa mali.
Kesi hiyo ilisababisha mvutano wa kidiplomasia kati ya Singapore na Marekani baada ya aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton kuingilia kati kuomba adhabu hiyo ipunguzwe.
Licha ya shinikizo kutoka Marekani, Singapore imesisitiza kuwa sheria zake lazima ziheshimiwe na watu wote, wakiwemo wageni.