Njombe. Madiwani wa halmashauri ya mji wa Njombe wamehoji na kutaka ufafanuzi kutoka ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhusu gharama iliyotumika kununua gari la maji taka ili kutoa huduma kwa wananchi baada ya kuliona kuwa na upungufu kadhaa.

Maelezo ya madiwani hao yanaonyesha kuwa gari hilo linatajwa kuwa jipya lakini baada ya kufanyiwa ukaguzi linaonekana ni la zamani na limepangwa rangi inayoonyesha kuwa ni jipya.

Hoja hizo zimetolewa leo Mei 9, 2026 na madiwani hao wakati wa kikao cha bara la madiwani kilichofanyika halmashauri ya mji wa Njombe wilayani humo.

Wamesema madiwani wanaishi kwenye jamii na kushirikiana na watu hivyo zipo taarifa walizoziskia kuhusu gari la maji taka lililonunuliwa na halmashauri hiyo kuwa siyo jipya.

Wamesema wanataka majibu ya gari nama 44215 aina ya FAW la maji taka ni muda mrefu lipo hapo halmashauri lakini kabla lilikuwa na rangi nyingine na sasa lina rangi nyingine.

Diwani wa kata ya Ramadhani, Erasto Ngole amesema mtaani kuna maneno yanayowaletea wasiwasi kuwa gari hilo kuna mchezo umefanyika wakati madiwani hao hawapo.

“Nataka kujua hili gari ni jipya au ni bovu? Na kama ni jipya limenunuliwa shillingi ngapi? Gari namba 44215,” amesema Ngole.

Amehoji, pia, gari namba 44149 kutaka kuja mahali lilipo na hali lililonalo kwa sababu thamani ya gari hiyo ni kubwa huku kwenye mitandao ya kijamii picha zikitembea kuonyesha gari hilo limepata ajali na kuharibika vibaya.

Amesema gari hilo halijanunuliwa muda mrefu na fedha zilizotumika ni za wananchi ambao wamekuwa wakitozwa ushuru wa mazao pamoja na kodi mbalimbali zilizowekwa na halmashauri hiyo.

Mbaya Zaidi, amesema licha ya kuwa taarifa hazijathibitishwa, wamesikia gari hilo limepata ajali mbaya kama ilivyoonekana kwenye picha lakini dereva aliyekuwa anaendesha wakati gari hilo linapata ajali hakuwa mtumishi wa halmashauri hiyo.

Amesema kama madiwani hao wataendelea kuonekana hawana meno kwa kufumbia macho matukio ya aina hiyo upo uwezekano wa halmashauri hiyo kwenda kufa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Erasto Mpete amesema baraza hilo la madiwani lina meno na halmashauri hiyo haiwezi kwenda kupotea hata kidogo na kama mwenye nia hiyo aondoke kwenye halmashauri hiyo.

Amesema kuhusu gari la maji taka lililalamikiwa na madiwani siyo jipya kwa sababu kupitia kamati ya fedha walipitia na kuona kasoro zilizoainishwa na kamati iliyoundwa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa ajili ya kukagua gari hilo.

“Ni kawaida kila gari likifika lazima kamati iundwe kukagua na kuthibitisha gari ni jipya? Kwa rosario zote zilizosemwa ishirini na kitu inatosha kuthibitisha hilo gari siyo jipya,” amesema Mpete.

Amesema wakati mwingine hakuna sababu ya kuunda kamati ili hali gari hilo kwa macho linaonekana siyo jipya ingawa malengo ya halmashauri hiyo ilikuwa kununua gari jipya.

Amesema mkataba wa kununua gari haukuzingatiwa hivyo maelekezo yalitolewa kwa mzabuni wa gari hilo kurudisha fedha au kuleta gari lingine jipya lakini mzabuni alileta gari lakini timu ilipoundwa tena ilibaini gari lilikuwa ni lile lile bali limebadilishwa rangi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Kuruthum Sadick amesema walipokea taarifa ya gari hilo lililoletwa mwezi wavkumi mwaka jana na Oktoba 23 aliunda kamati baada kulipitia gari hilo na kuona lina changamoto.

Amesema aliita wataalamu kutoka Temesa na kushirikiana na wataalamu wa halmashauri kama sheria inavyosrma baada ukaguzi taarifa ilitolewa kuwa gari hilo lina mapungufu.

“Upungufu wote tuliweza kuyaorodhesha na ilipofika Novemba waliridhia huo upungufu kwamba gari hili hatulitaki watuletee gari jipya,” amesema Sadick.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *