Unguja. Fedha kiduchu zinazotengwa na kutolewa kwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Taasisi zake zimeibua mjadala kwa wawakilishi wakiitaka Serikali kuangalia upya mipango yake kwani taasisi zote zinazosimamiwa na ofisi hiyo zinafanya kazi ambazo zipo kwenye mapambano ya kidunia.

Wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya ofisi hiyo barazani hapo Chukwani Unguja, baadhi ya wajumbe hao wamesema ofisi hiyo inapambana na mambo makubwa yenye athari kiulimwengu, lakini inasikitisha kuona fedha zinazotengwa na kutolewa haziwezi kuleta matokeo yoyote.

Mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar (ACT Wazalendo), amesema kulingana na majukumu ya ofisi hiyo, fedha zinazotengwa zitolewe kwa asilimia 100, lakini imekuwa kinyume chake.

“Kwakweli jambo hili linasikitisha, ukiangalia hii dio ofisi yenye taasisi zinazopambana na mambo makubwa ya Ukwimi, Dawa za Kulevya, Mazingira (mabadiliko ya tabianchi) na Watu Wenye Ulemavu, inapangiwa fedha licha ya kuwa kidogo, lakini bado zinatolewa chache,” amesema mwakilishi huyo

Akitolea mfano katika idara ya mazingira inayosmamia mabadiliko ya tabianchi ambapo kwa mwaka 2025/26 ilipangiwa Sh6.4 bilioni, lakini hadi kufikia Machi 30 zimetolewa Sh1.4 bilioni sawa na asilimia 19.

Kwa upande wa watu wenye ulemavu, walipangiwa Sh1.5 bilioni lakini zimetolewa Sh700 milioni huku taasisi ya dawa za kulevya ilipangiwa Sh7.7 bilioni na zimetolewa Sh2.4 bilioni sawa na asilimia 31.

“Tukitaka kupambana na haya, lazima tuweke utashi wa kisiasa na kutoa kipaumbele kwa taasisi hizo,” amesema mwakilishi huyo.

Mwakilishi nafasi za Wanawake, Jabu Makame Juma alichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais barazani Chukwani Unguja Zanzibar

Hata hivyo, amesema kinachosababisha tatizo hilo ni kupanga bajeti kwa kutegemea wafadhili kwa hiyo wasipotoa fedha hizo inabaki pengo kubwa hivyo akashauri, umefika wakati Serikali kutafuta vyanzo vipya vya mapato badala ya kuendelea kusubiri wafadhili.

Mwakilishi wa nafasi za Wanawake (CCM), Aza January amesema mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi yanahitaji fedha, kwa hiyo licha ya fedha hizo ndogo zinazotengwa na kupitishwa Barazani taasisi husika zinatakiwa zipewe fedha zote.

Mwakilishi wa Chaani, Juma Usonge Hamad amesema bajeti ni ndogo inatakiwa iongezwe ili kusaidia programu zake.

“Tuongeze bajeti ya hii wizara kwa sababu inapambana na dawa za kulevya, sote tunajua jinsi dawa za kulevya zinavyohusisha watu wakubwa wenye fedha nyingi na maeneo yanayohusika kupitisha hizi dawa yanahitaji makakti wa kifedha nyingi,” amesema Usonge

Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayub (CCM) amesema bado watu wenye ulemavu wanapitia changamoto nyingi kwa kutengewa fedha kidogo lakini zinazotoka pia haziridhishi huku wakiwa na gari moja la kutumia.

“Fedha nyingi zinatoka kwa wafadhili, kwanini hapa Serikali inatia fedha kidogo?” amehoji Jaku.

Kwa upande wa mazingira Jaku amesema hali hairidhishi kwani katika maeneo ya Pwani uchafu ni mwingi kupindukia.

Akichangia upande wa programu ya Ukimwi, Jaku amesema Ukimwi unachangiwa na kuongezeka kwa utitiri wa baa kila kona jambo linalochangia tatizo hilo.

“Enzi za wakoloni hapa Zanzibar mtu alikuwa hawezi kulewa bila ya kibali, kwa hiyo sheria ya vileo inahitaji kufanyiwa marekebisho,” amesema.

Naye Jabu Makame Juma (nafasi za wanawake), amesema serikali  lazima iwekeze nguvu kubwa kwa watu wenye ulemavu na mfuko wao uongezwe na itambue mahitaji yao.

“Serikali iwe na mikakati na sheria mathubuti kupambana na dawa za kulevya, tuangalie analeta nani hizi dawa na madhara makubwa wanapata vijana wetu,” amesema

Akihitimisha mjadala kwa kujibu hoja hizo za wawakilishi, Kaimu Waziri Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Hamza Hassan Juma amesema wamepokea maoni yote na ushauri hivyo Serikali itakwenda kuufanyia kazi lengo ni kutaka kuona mabadiliko ya katika ustawi wa jamii.

Baraza hilo limepitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa kuhidhinisha kwa mwaka wa fedha 2026/27  Sh35.558 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh17.529 bilioni kwa matumizi ya kawaida ambapo Sh7.453 bilioni kwa ajili ya mishahara, Sh8.223 bilioni kwa matumizi mengineyo, na ruzuku Sh1.906 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *