Dar es Salaam. Uelewa wa kutumia taka kama fursa ya biashara katika kuzalisha bidhaa bado ni mdogo miongoni mwa wananchi, jambo linaloifanya Serikali kuja na mkakati maalumu.

Hayo yamesemwa Mei 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya Mazingira ambayo huadhimisha kila mwaka ifikapo Juni 5.

Kwa mujibu wa Masauni, Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 12.1 hadi 17.4 za taka ngumu kwa mwaka na zinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia tani milioni 30 hadi 60 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.

“Asilimia 60 hadi 75 ya kiasi cha taka ngumu kinachozalishwa ni taka oza na asilimia 10 hadi 15 ni taka rejelezi ikiwamo plastiki, karatasi, aluminiamu, glasi, taka za kielektroniki na chuma chakavu.

“Hivyo, kiasi cha taka oza kinachozalishwa kwa mwaka ni takribani tani milioni 9.9 ambapo ni asilimia ndogo tu hurejelezwa,” amesema Waziri huyo.

Katika mikakati wanayokuja nayo, Masauni amesema moja ya mambo watakayoyafanya ni kutoa elimu ya matumizi ya taka kuwa bidhaa na sio kama mzigo.

“Nataka nikubaliane kwamba licha ya taka kuwa ni fursa lakini katika nchi yetu bado hatujaweza kuitumia ipasavyo jambo linalochangiwa pia na uelewa mdogo kwa jamii,” amesema.

 “Nimeshuhudia taasisi, kampuni zikizalisha bidhaa kupitia taka ambapo wapo waliozalisha kwa kiwango cha chini cha kati na cha juu, hali inayoonyesha uwezo wa kutumia taka kuzalisha bidhaa Tanzania upo”.

“Hivyo, kupitia mkakati huo tunaenda kutatengeneza ajira nyingi kwa vijana kupitia utengenezaji wa bidhaa kutokana na taka tunazozilisha,” amesema.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho siku ya mazingira, amesema kwa mwaka huu yatafanyika mkoani Dodoma huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema wakati kaulimbiu ya kimataifa itakayoongoza maadhimisho hayo ni “Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Vitendo”, kitaifa kaulimbiu ni “Dira 2050: Tuwajibike kukijanisha Tanzania”.

Kaulimbiu hiyo, amesema inahimiza jamii ya Watanzania kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Jitihada hizi lazima ziwe sehemu ya safari ya maendeleo ya muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kukijanisha Tanzania, kuongeza jitihada katika kulinda misitu yetu na kupanda miti kwa wingi.

“Jingine ni kutumia nishati safi ya kupikia, ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia yameendelea kuongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 28.6 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia mwaka 2025,” amesema.

Hata hivyo, amesema kaulimbiu hiyo ya kitaifa inatafsiri kwa vitendo, wito wa kaulimbiu ya kimataifa kwamba kila Mtanzania anapaswa kuchukua hatua sasa ili kuhakikisha kuwa maendeleo tunayoyapata hayaathiri mazingira na maisha ya vizazi vijavyo.

Kaulimbiu ya kimataifa inasema “Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Vitendo” lengo likiwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza kasi na juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesijoto, kukuza matumizi ya nishati mbadala, na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Kwa pande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Richard Muyungi amesema kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha kituo chake cha kuchakata hewa ya kaboni licha ya hatua hizo kwenda taratibu tayari wameshakijengea uwezo kwa kuwa na bodi na menejimenti yake.

“Kituo hiki tumeshakipa nyenzo na ofisi yao itakuwa ya kudumu pale Mtumba, Dodoma.

Dk Muyungi amesema wamejiwekea malengo ya kuwa na fedha za kuchangia pato la Taifa katika kutekeleza Dira ya 2050, fedha ambazo zitatokana na biashara ya kaboni.

“Ndio maana wanakiimarisha kituo hicho pamoja na kukiwekea programu za muda mfupi na mrefu kuhakikisha kinakuwa muhimu kwa nchi na Afrika kwa ujumla,” amesema Dk Muyungi.

Ukiacha kituo hicho, amesema pia wanatarajia kuzindua kituo cha majanga ambapo itakuwa ofisi ya kwanza ya Umoja wa Mataifa hapa nchini itakayosaidia katika changamoto za majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *