Dar es Salaam. Wafanyabiashara nchini wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mikutano na makongamano ya kimataifa ili kupata masoko mapya, washirika wa biashara na fursa za uwekezaji.

Wito huo umetolewa leo Mei 12, 2026 jijini Dar es Salaam na Rais wa Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC), Vicent Minja, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu makubaliano ya ushirikiano (MoU) yaliyofikiwa kati ya chemba hiyo, Cchemba ya biashara ya Kenya na ya Zanzibar.

Minja amesema mwitikio wa wafanyabiashara wa Tanzania katika makongamano ya biashara bado ni mdogo tofauti na wenzao wa Kenya, jambo linalokwamisha upanuzi wa masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi.

Amesema Tanzania inaendelea kuvutia wawekezaji wengi, lakini wafanyabiashara wa ndani wanapaswa kutumia vyema fursa hizo kwa kushiriki majukwaa ya biashara na kujitangaza kimataifa.

“Bidhaa nyingi zinazozalishwa hapa nchini zina ubora mkubwa, lakini zinakosa masoko kwa sababu wafanyabiashara wa nje hawana taarifa kuhusu uwepo wake,” amesema.

Ametoa mfano wa bidhaa kama nondo na vioo zinazozalishwa kwa wingi nchini huku baadhi ya wafanyabiashara wa nchi jirani wakiendelea kuziagiza kutoka mataifa ya mbali kutokana na ukosefu wa taarifa.

Aidha, amesema TNCC itaendelea kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa kimataifa, huku makubaliano yaliyofikiwa na Kenya yakihusisha kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi ndani ya siku 90 na kuanzisha mfumo wa pamoja wa utatuzi wa migogoro ya biashara.

Minja pia amewahamasisha vijana kujiunga na TNCC ili kupata mafunzo, uzoefu na mitandao ya biashara itakayowasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TNCC, Matina Nkurlu, amesema bado vijana wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa chemba hiyo, hivyo wanaendelea kutumia mitandao ya kijamii, vyuo na makongamano kuwafikia vijana wengi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *