Ilikuwa mwaka 1994. Alikuwa na umri wa miaka 13. Akamshuhudia baba yake akiuawa. Ni matokeo ya mauaji ya Kimbari Rwanda. Chuki za Wahutu na Watutsi. Jumlisha uroho na ulafi wa madaraka. Watu milioni 1.2 waliuawa.

Mtoto akabaki yatima. Akavuka mpaka hadi Burundi. Akaishi na ndugu. Akataka kujiunga na kikundi cha waasi cha RPA ili alipe kisasi cha kifo cha baba yake. Akakosa njia ya kujiunga na kundi hilo. Mwaka huohuo, hali ilipotulia, alirejea Rwanda.

Alipomaliza shule ya juu (high school), alijiunga na masomo ya dini. Yule mtoto akawa kijana. Akawa mhubiri wa neno la Mungu.

Zile chuki na roho ya kisasi vikaondoka. Akaeneza Injili. Kipaji chake cha kuimba nyimbo za Injili, kikampa umaarufu.

Mwaka 2001, akaanzisha Taasisi Isiyo ya Kiserikali (NGO) ya Maridhiano. Alihubiri upatanisho na msamaha kwa Wahutu na Watutsi. Mwaka huohuo, kijana Muinjilisti alishiriki kutunga na kuimba wimbo wa taifa la Rwanda. Kwa ushiriki huo, alipewa zawadi na Rais Paul Kagame kwenda kusoma nchini Ufaransa.

Kijana Muinjilisti alirejea Rwanda baada ya masomo. Akaendelea kutangaza Injili kwa nyimbo na mahubiri. Akawa kijana pendwa wa Serikali. Alishiriki matukio mengi ya Serikali.

Mwaka 2010, kijana Muinjilisti aliitanua taasisi yake ya amani na maridhiano, akaiita KMP Foundation. Akaendelea kufanya kazi ya Mungu na kijamii. Ungemuona pichani na Rais Kagame au mke wa rais, Jeannette Kagame, akimpa tuzo ya kazi nzuri ya kueneza amani.

Mwaka 2014, kijana Muinjilisti alivuka mstari mwekundu, akatoa wimbo wa Kinyarwanda “Igisobanuro cy’Urupfu”, maana yake ni Tafsiri ya Kifo.

Japo yeye ni Mtutsi, aliimba kuikosoa Serikali kueneza propaganda kuhusu mauaji ya Kimbari, kwamba Watutsi ndiyo waliuawa, wakati Wahutu wengi pia waliuawa na wanapaswa kukumbukwa.

Wimbo huo ukapigwa marufuku Rwanda. Kijana Muinjilisti akageuka adui. Akashtakiwa kwa kula njama za kumuua Rais Kagame. Mwaka 2015 alihukumiwa kifungo jela miaka 10.

Mwaka 2018 aliachiwa kwa msamaha wa Rais. Februari 14, 2020, ilikuwa Ijumaa, kijana alikamatwa.

Alidaiwa alitaka kuvuka mpaka kwenda kujiunga na vikundi vya waasi. Aliwekwa mahabusu. Februari 17, 2020, ilikuwa Jumatatu, ikaripotiwa kuwa kijana alijiua akiwa mahabusu.

Ni simulizi kuhusu Muinjilisti wa Kikatoliki, Kizito Mihigo. Hadithi yake duniani ilikatika alipokuwa na umri wa miaka 40. Nusu ya umri wa maandiko kwenye Biblia, unaosema binadamu ataishi duniani kwa miaka makumi manne mawili.

Kwa nini nimemkumbuka Kizito leo?

Mei 6, 2026, Jumatano iliyopita, kiliripotiwa kifo Rwanda kinachofanana na kile cha Kizito. Ni kuhusu Aimable Karasira, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Rwanda na mtengeneza maudhui wa mitandaoni, hasa YouTube.

Karasira alipoteza maisha akiwa Hospitali ya Wilaya ya Nyarugenge, Kigali.

Mshangao ni kuwa mauti yalimfika Karasira muda mfupi kabla kuachiwa huru. Maana tayari alikuwa amemaliza kifungo chake cha miaka mitano jela. Taarifa ya Jeshi la Magereza Rwanda (RCS), ilieleza kuwa Karasira alitumia kiasi kikubwa cha dawa, kilichosababisha mauti yake.

RCS waliongeza kuwa Karasira alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya shinikizo la juu la damu, kisukari na mdororo wa afya ya akili, kwa hiyo alipokuwa akisindikizwa na askari wa magereza, kutoka nje ya gereza la Nyarugenge, alibugia kiasi kikubwa cha dawa, hivyo kumsababishia umauti.

Kesi ya Karasira ni ileile. Kukosoa nadharia ya Mauaji ya Kimbari Rwanda mwaka 1994. Serikali ya Rwanda imekuwa ikiyapa utambulisho Mauaji ya Kimbari Rwanda kuwa yalikuwa mauaji dhidi ya Watutsi. Utambulisho huo wa Serikali ya Rwanda umekuwa ukikosolewa vikali na wanaharakati pamoja na watoa maoni wa kawaida.

Wakosoaji wamekuwa wakitoa msimamo kuwa Mauaji ya Kimbari Rwanda yaliathiri jamii zote, Wahutu na Watutsi. Kutamka hadharani kuwa Wahutu waliuawa Rwanda mwaka 1994, limekuwa kosa la jinai, ambalo kwa sheria za nchi hiyo ni sawa na kukana kuwa mauaji ya kimbari hayakuwepo (Genocide Denial Act). Sheria namba 18 ya mwaka 2008, kama ilivyoboreshwa mwaka 2018.

Sheria hiyo, kwa Rwanda, inataka watu wote kukubali kuwa Mauaji ya Kimbari Rwanda mwaka 1994, yalikuwa mauaji dhidi ya Watutsi. Ukikosoa unakuwa umetenda kosa la jinai, ambalo adhabu yake ni kifungo jela na kulipa faini kubwa.

Karasira alitokeza hadharani na kueleza kuwa yeye ni shuhuda kuwa ndugu zake, jamii ya Wahutu, waliuawa na RPF (Rwanda Patriotic Front), wakati huo kikiwa kikundi cha waasi. Hivi sasa, RPF ndiyo jeshi la Rwanda.

Maelezo ya Karasira, yalikuwa kuunga mkono hoja za wakosoaji wengi kwamba RPF chini ya Kagame, ilihusika moja kwa moja na Mauaji ya Kimbari Rwanda mwaka 1994. Hata hivyo, baada ya RPF kuipindua serikali iliyokuwapo na kushika hatamu, iliamua kutengeneza hadithi inayoonesha kuwa waliouawa walikuwa Watutsi peke yao.

Asili ya Mauaji ya Kimbari Rwanda mwaka 1994, chanzo chake ni mauaji ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana, aliyetunguliwa akiwa kwenye ndege, wakati alipokuwa anakaribia kutua Uwanja wa Ndege wa Kigali.

Habyarimana, aliuawa pamoja na aliyekuwa Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira. Ndege ya Rais wa Rwanda, iliyokuwa imewabeba Habyarimana na Ntaryamira, ilitunguliwa na RPF. Mauaji ya viongozi hao, yalichochea mauaji ya kikabila, Wahutu na Watutsi. Serikali ya Rwanda chini ya Kagame haitaki itamkwe kwamba Wahutu pia waliuawa.

Septemba 2019, aliyekuwa ofisa mwandamizi wa Ofisi ya Rais wa Rwanda, Kalisa Mupende, alifariki dunia akiwa gerezani, ni baada ya kuvuka mstari hatari dhidi ya Kagame. Pamoja na matukio mengine ya wakosoaji wa Kagame kupoteza maisha kitatanishi, matukio hayo yamekuwa yakilichora jina la Kagame kwa wino wa damu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *