Ni kushambulia mwanzo mwisho. Hiyo ni kauli ya Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa akielezea maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa kesho Alhamisi Mei 14, 2026 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Nsajigwa ambaye ameiongoza timu hiyo kwa michezo tisa bila ushindi, presha imeonekana kuwa kubwa nje na ndani ya uwanja katika hesabu za kukwepa kushuka daraja.

Katika michezo 22 iliyocheza timu hiyo ya jijini Mbeya, imekusanya pointi 14 na kuwa nafasi ya 15 ambapo inahitaji ushindi mechi zilizobaki kujihakikishia kubaki salama Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa amesema baada ya kusota kwa muda mrefu bila kupata pointi tatu, kesho huenda ikawa safari ya matumaini mapya watakapoilaza Fountain Gate na kuianza upya Ligi Kuu, huku akitoa angalizo kwa nyota wa kikosi chake.

Amesema baada ya kufanikisha kutengeneza muunganiko na unyumbulifu kwa timu katika kutengeneza nafasi bila kuzitumia vyema, amewaandaa vizuri wachezaji kuhakikisha kesho wanafanya kweli.

“Tumeshafungwa sana, ila sisi hatujashinda, kesho ni kushambulia tu kusaka mabao na kulinda pointi tatu, vijana nimewaandaa kiakili, kimbinu na kiufundi ili tuianze upya safari ya matumaini.

“Tunajua rekodi na historia yetu nyuma kwamba kila msimu huwa tuna mechi zinazotubeba hadi kubaki, hivyo hatujakata tamaa na tunaweza kubaki salama, ila lazima tushinde michezo hiyo,” amesema kocha huyo.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Fred Felix ‘Minziro’ amesema wanafahamu mchezo huo ugumu wake kutokana na wapinzani walivyo akisisitiza kuwa timu hiyo pia haijawa salama, hivyo lazima kupambania walichonacho kwa sasa.

Amesema ushindi na matokeo waliyopata katika mechi zilizopita hadi kuwa nafasi ya 10 kwa pointi 25, haiwafanyi kubweteka bali kulinda mwendelezo huo ili kukwepa kushuka daraja.

“Wachezaji wako tayari kwa mchezo na sisi hatuko salama sana, tunaenda kwa nidhamu, heshima na tahadhari katika mchezo huo kwa kuwa Prisons ni timu nzuri, ukifanya makosa wanakuadhibu,” amesema kocha huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *