Musoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimebainisha kuwa  kitawachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wanachama watakaoendelea kuonyesha kutoridhishwa na maamuzi ya chama kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali uliofanyika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Onyo hilo limetolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Kenani Kihongosi wakati akizungumza na wanachama wa CCM wa shina namba tano Tawi la Mwisenge mjini Musoma leo Mei 14, 2026.

Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na taarifa za kuwepo kwa mpasuko ndani ya chama hicho katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Mara, hali inayodaiwa kuchangiwa na tofauti zilizojitokeza wakati wa kura za maoni za ndani ya chama.

Akizungumza katika mkutano huo, Kihongosi amesema maamuzi yaliyofanywa na vikao vya CCM katika uteuzi wa wagombea yalifuata kanuni, taratibu na misingi ya chama, hivyo yanapaswa kuheshimiwa na kila mwanachama.

“Maamuzi ya chama lazima yaheshimiwe na watu wote. Hakuna aliye mkubwa kuliko chama. Wale wote walioteuliwa walikuwa na sifa zinazostahili kwa nafasi walizopewa,” amesema Kihongosi.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza na wanachama wa CCM shina namba tano tawi la Veta Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Amesema chama hicho hakitakuwa tayari kuona baadhi ya watu wakikiuka maamuzi kwa masilahi binafsi au kuendeleza migogoro inayoweza kudhoofisha mshikamano ndani ya CCM.

“Yeyote atakayekwenda kinyume na maamuzi ya chama atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za chama. Hatuko tayari kuona chama kinaharibiwa na watu wachache,” amesema.

Kihongosi amewataka wanachama wa CCM mkoani Mara kuendelea kushikamana na kutoa ushirikiano kwa viongozi walioteuliwa, badala ya kuendeleza makundi yanayoweza kuathiri utekelezaji wa shughuli za chama.

Amesema CCM imekuwa na utaratibu wa kidemokrasia wa kupata viongozi tangu kuanzishwa kwake, huku akitolea mfano namna viongozi wakuu wa chama walivyokuwa wakikabidhiana madaraka kwa utaratibu bila migogoro.

Amefafanua kuwa  kuanzia enzi za Julius Nyerere hadi sasa, CCM imeendelea kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia katiba, kanuni na mshikamano wa chama.

“Huo ndiyo msingi wa chama chetu. Kila kiongozi anapomaliza muda wake hukabidhi kijiti kwa anayefuata bila migogoro. Hivyo wanachama wanapaswa kuendelea kuheshimu misingi hiyo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *