Dar es Salaam. Ukurasa mpya wa uwekezaji unatarajiwa kufunguliwa nchini kupitia mkutano wa uwekezaji Tanzania wa mwaka 2026, utakaoleta pamoja wawekezaji na wadau wakubwa duniani huku miradi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.85 sawa na Sh7.4 trilioni za Kitanzania ikitangazwa kwa wawekezaji hao wa ndani na nje ya nchi.
Pia, katika mkutano huo uliotangazwa rasmi leo Mei 14, 2026 ambao hadi sasa wawekezaji zaidi ya 70 kutoka nchi hizo za maabara ya Asia, Amerika na Ulaya, wameshajiandikisha kuja una lengo la kuunganisha wawekezaji wa kimataifa, taasisi za fedha pamoja na waendelezaji wa miradi na miradi ya uwekezaji iliyo tayari kutekelezwa.
Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya Tanzania Investment Growth Facility (TIGF) kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) unatarajiwa kufanyika Juni mosi hadi 2, 2026 jijini Arusha.
Akizungumzia mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji taasisi ya ESRF, Profesa Fortunata Makene amesema lengo kuu ni kuhakikisha miradi ya uwekezaji inapata ufadhili na kuingia katika utekelezaji badala ya kubaki katika hatua ya majadiliano.
“Miradi 60 iliyotayarishwa kwa ajili ya uwekezaji inahusisha sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo utalii na miundombinu ya hifadhi za asili, nishati jadidifu, usafirishaji na logistiki, uchumi wa buluu, uchakataji wa mazao ya kilimo, miundombinu ya maji pamoja na miradi ya maendeleo ya serikali za mitaa,” amesema.
Profesa Makene amesema Tanzania ipo tayari kubadilisha fursa hizo kuwa miradi yenye uwezo wa kupata ufadhili wa kifedha.
“Tanzania ipo tayari ikiwa na miradi iliyofanyiwa uchambuzi, ushirikiano wa Serikali, uungwaji mkono wa taasisi pamoja na mifumo ya kuwezesha majadiliano halisi ya uwekezaji. Hili ni jukwaa ambalo wawekezaji wa kimataifa wanaweza kutumia kupata fursa hizi,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji taasisi ya ESRF, Profesa Fortunata Makene akizungumza leo jijini Dar es salaam kuhusu mkutano mkubwa wa uwekezaji wa (Tanzania Investment Summit 2026) utakaofanyika jijini Arusha. Picha na Sute Kamwelwe.
Ameongeza waandaaji watafuatilia kila ombi la uwekezaji na kusaidia mradi hadi kufikia hatua ya kufungwa kwa makubaliano ya kifedha huku akisema wadau watafanya makubaliano mbalimbali ya miradi ya Serikali katika maeneo ya miundombinu, uchumi wa buluu na utalii.
“Miradi ya Serikali ipate pesa kutoka kwa wadau hao na kuiweka Tanzania kama nchi salama ya uwekezaji ambapo katika mkutano huo mgeni rasmi ni profesa Kitila Mkumbo Waziri wa Mipango na Uwekezaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara, amesema sekta binafsi ina nafasi muhimu katika hatua mpya ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Mitaji binafsi inayopatikana, dhamana za kifedha pamoja na mifumo ya kugawana hatari ndiyo msingi wa sura mpya ya ukuaji wa Tanzania,” amesema Komatsubara.
Waandaaji wa mkutano huo wamesema wanatarajia kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa wawekezaji katika kundi la awali la miradi kati ya minane hadi 10 yenye kipaumbele na thamani ya dola za Marekani milioni 100, ambayo inatarajiwa kuwa hatua ya kwanza ya makubaliano ya uwekezaji.
Kadhalika, mkutano huo utakuwa kichocheo muhimu cha kuongeza uwekezaji endelevu nchini na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama moja ya vituo vikuu vya uwekezaji barani Afrika.
Kupitia mkutano huo, Tanzania inalenga kuongeza kasi ya uwekezaji wa kimataifa na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.