Bado pointi mbili! Hivyo ndivyo mashabiki wa Simba wanavyotamba kwa sasa baada ya kuona kuna tofauti ndogo sana dhidi ya Yanga iliyo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa, jana Alhamisi.

Simba imepunguza tofauti ya pointi kutoka tano hadi mbili kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma kufuatia mabao yaliyofungwa na Clatous Chama aliyeendeleza balaa katika mchezo wa nne mfululizo akitupia.

Kama ilivyokuwa katika michezo iliyopita, kocha wa Simba, Steve Barker aliamua kuendelea kuanza bila ya mshambuliaji wa kati halisi huku nafasi hiyo akicheza Elie Mpanzu ambaye amekuwa na maelewano mazuri na Chama.

Katika dakika ya sita tu ya mchezo, Chama aliwapa raha mashabiki wa Simba kufuatia kuchonga kona iliyozama moja kwa moja na kumuacha kipa wa Mashujaa, Patrick Munthali akilalamika.

Baada ya kuwa mbele kwa bao 1-0, Simba iliendelea kulisakama lango la Mashujaa lakini walishindwa kufungua ukuta wa timu hiyo ambao ulikuwa ukiongozwa na Samson Madeleke na Mohamed Salum.

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Simba ilikuwa na shuti moja ambalo lililenga lango sawa na Mashujaa ambayo shuti lao halikulenga lango la Wekundu hao wa Msimbazi.

Mashujaa ikiongozwa na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ilirejea kipindi cha pili na kufanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwa mpigo kwa kuwatoa Salum Kihimbwa, Baraka Mtuwi na Mgandila Shabani huku wakiingia Crispin Ngushi, Balama Mapinduzi na Yusuf Dunia.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwapa nguvu Mashujaa ambao walianza kujibu mapigo ikisaka bao la kusawazisha.

Miongoni mwa wachezaji wa Mashujaa ambao walionekana kuisumbua Simba ni Ismail Mgunda ambaye kidogo aifungie Mashujaa bao la kusawazisha kufuatia kuachia mkwaju uliogonga nguzo na mpira huo kuondoshwa haraka katika eneo la hatari.

Baada ya kuona Mashujaa wamefunguka, kocha wa Simba, Steve Barker aliamua kufanya mabadiliko ya kimkakati katika dakika ya 61 kwa kumtoa Inno Loemba na kuingia Anicet Oura ili kuongeza kasi na ubunifu katika maeneo ya pembeni.

Katika dakika ya 70, Simba ilipata bao la pili lililofungwa na Chama akimaliza pasi ya Mpanzu na kumfanya kufikisha bao la nane msimu huu wa Ligi Kuu Bara huku akifunga katika mechi nne mfululizo.

Seleman Mwalimu alihitimisha ushindi huo kwa bao la dakika ya 90+1. Hilo ni bao la nane kwa Mwalimu ndani ya ligi msimu huu.

Matokeo hayo yameifanya Simba kuendeleza ubabe wake dhidi ya Mashujaa kwa kushinda mechi sita mfululizo katika ligi pia wameifanya timu hiyo ya Kigoma kupoteza mechi ya kwanza nyumbani msimu huu.

Simba imesaliwa na mechi saba ambazo ni dhidi ya Coastal Union (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), Pamba Jiji (nyumbani), Mbeya City (ugenini), Mtibwa Sugar (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani) na KMC (nyumbani).

Prisons yapata ushindi

Katika mechi zilizochezwa mapema, Tanzania Prisons ilimaliza mfululizo wa mechi tisa bila ya kupata ushindi baada ya kuibuka na kuichapa Fountain Gate bao 1-0 lililofungwa na George Mpole katika dakika ya 25 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kabla ya ushindi huo muhimu, Prisons ilikuwa imepoteza michezo saba huku ikitoa sare mbili katika mechi tisa zilizopita, matokeo yaliyowaweka maafande hao kwenye hatari ya kushuka daraja.

Licha ya ushindi huo, Prisons imeendelea kusalia katika nafasi ya 15 moja kutoka mkiani ikiwa na pointi 17.

Mtibwa yaweka rekodi

Mabao saba yaliyofungwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro wakati wenyeji Mtibwa Sugar wakiibuka na ushindi wa 4-3 dhidi ya KMC, yameweka rekodi ya kuwa mchezo wenye mabao mengi zaidi katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara hadi sasa.

Kabla ya mchezo huo, rekodi ya mabao mengi kwenye mechi moja ilikuwa ikishikiliwa na Yanga baada ya kuichapa Mbeya City mabao 6-0, Aprili 16 mwaka huu, pamoja na ushindi mwingine wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa Januari 19 mwaka huu. Mechi hizo mbili zilikuwa zimezalisha mabao sita kila moja kabla ya rekodi hiyo kuvunjwa Morogoro.

Mbali na kuweka rekodi hiyo, ushindi huo umeongeza matumaini kwa Mtibwa Sugar katika mapambano ya kusalia Ligi Kuu Bara wakifikisha pointi 26 katika nafasi ya 10 huku KMC ikiendelea kusuasua ikibaki na pointi tisa mkiani mwa msimamo baada ya kupoteza mchezo mwingine licha ya kufunga mabao matatu ugenini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *