Dar es Salaam. Mrembo na mfanyabiashara maarufu mitandaoni, Poshy Queen, ameonekana kubadilika siku za karibuni baada ya kuamua kuyaweka pembeni maisha ya ‘kelele za mitandaoni’ na kuishi kwa utulivu zaidi tangu aingie kwenye ndoa.

Tofauti na zamani ambapo jina lake lilikuwa halikosekani kwenye kurasa za burudani kutokana na mahusiano, picha za kifahari na mijadala ya kimapenzi. Kwa sasa Poshy Queen ameonekana  kuwa kimya zaidi, hali iliyowafanya mashabiki wengi kuamini kuwa ndoa imempa utulivu  wa maisha.

Akizungumza na Mwananchi, Poshy Queen amesema maisha yake ya sasa ni tofauti na yale aliyokuwa akiishi zamani, huku akieleza kuwa ndoa imemfanya kuwa mtulivu zaidi na kuanza kuangalia maisha kwa mtazamo mpya.

“Kila hatua ya maisha ina wakati wake. Kwa sasa nimetulia sana tofauti na zamani. Ndoa imenifanya niwe na amani zaidi na nijikite kwenye maisha yangu binafsi kuliko kelele za mitandaoni,” amesema Poshy Queen.

Kauli hiyo imekuja kipindi ambacho mashabiki wengi wamekuwa wakijiuliza alipo Poshy Queen baada ya kupungua kwa hekaheka zake kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwa mrembo huyo.

Poshy Queen aliwahi kuwa gumzo alipokuwa kwenye uhusiano na msanii wa Bongofleva, Harmonize ambapo wawili hao walikuwa wakitajwa mara kwa mara kwenye habari za burudani kutokana na penzi lao lililokuwa likifuatiliwa kwa karibu na mashabiki.

Mahusiano yao yaliyoanza Januari 2024 yaliambatana na picha, video pamoja na matukio mengi yaliyokuwa yakizua mjadala mkubwa mtandaoni, lakini baadaye yakafikia mwisho huku kila mmoja akiendelea na maisha yake.

Katika moja ya mahojiano yake ya Agosti 16, 2024, Poshy Queen alifunguka kuhusu changamoto za maisha yake ya mapenzi, ikiwemo kuvunjika kwa ndoa yake ya kwanza aliyofunga 2020 na raia wa Nigeria.

“Niliolewa mwaka 2020 na nilikaa kwenye ndoa mwaka mmoja na nusu. Chanzo kikubwa cha kuachana kilikuwa utofauti wa mila zetu lakini pia suala la umbali kati yetu,” alieleza.

Mbali na hilo, Poshy Queen pia aliwahi kuzungumzia migogoro iliyokuwa inayomhusu na Harmonize, akisisitiza kuwa mengi yaliyokuwa yakisemwa mitandaoni hayakuwa na ukweli.

“Mimi na Harmonize hatukugombana kwa sababu ya kauli za mpira kama watu walivyokuwa wanasema. Changamoto zilizokuwepo zilikuwa za kawaida kwenye mahusiano na si kila kinachoandikwa mtandaoni ni kweli,” alisema.

Hata hivyo, baada ya kuachana na Harmonize, maisha ya Poshy Queen yalionekana kubadilika ghafla. Mrembo huyo alianza kupunguza uwepo wake kwenye mitandao na baadaye akaja kuthibitisha kuwa ameolewa na mwanaume anayejihusisha na shughuli za udalali.

Hatua hiyo iliwashangaza wengi, hasa kutokana na namna ambavyo alikuwa akiishi maisha ya wazi zaidi kipindi cha nyuma. Wapo waliodhani huenda asingetulia kirahisi, lakini kwa sasa mambo yanaonekana kwenda tofauti kabisa.

Mashabiki wake wengi wamekuwa wakisema ndoa imembadilisha kwa kiasi kikubwa, huku wengine wakieleza kuwa utulivu wake wa sasa unaonyesha ameamua kuanza ukurasa mpya wa maisha bila presha ya umaarufu wa mitandaoni.

Mmoja wa mashabiki wake aliandika kuwa: “Poshy wa sasa ni tofauti kabisa na yule wa zamani. Inaonekana kweli ameamua kutulia.”

Wengine wameendelea kumpongeza kwa maamuzi yake ya kuweka maisha yake binafsi mbali na mitandao, wakisema si kila mtu maarufu anaweza kufanya hivyo kwa urahisi.

Kwa sasa, licha ya kupunguza makelele ya mitandaoni, Poshy Queen bado anaendelea kufanya biashara zake huku akionekana kuishi maisha ya utulivu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani.

Na wakati wengi wakiendelea kukumbuka enzi za mahusiano yake yaliyotikisa mitandao, hasa akiwa na Harmonize, ukweli unaoonekana sasa ni kwamba mrembo huyo ameanza safari mpya ya maisha ambayo imejaa utulivu, faragha na amani zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *