Mfumo wa ubunifu wa masuala ya tabianchi nchini Tanzania umechukua hatua muhimu mbele kufuatia kufanyika kwa maonyesho ya ubunifu wa tabianchi (Climate Innovation Expo) yaliyowakutanisha wabunifu, wawekezaji na wadau wa maendeleo jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lililofanyika Aprili 22, 2026 kwa ushirikiano na SmartLab, lilihudhuriwa na washiriki 180 limeweka suluhisho bunifu za ndani katikati ya juhudi za kukabiliana na changamoto za tabianchi huku likifungua fursa za ukuaji na upatikanaji wa mitaji.
Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja wajasiriamali bunifu na mashirika 26 yanayoongozwa na vijana yaliyowasilisha suluhisho katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, nishati safi, uchumi mzunguko, usimamizi wa maji pamoja na uchumi wa buluu. Ubunifu huo unaonesha kukomaa kwa sekta ya ubunifu nchini, ambapo mawazo yanabadilika na kuwa suluhisho halisi zenye uwezo wa kupanuka.
Maonesho hayo pia yaliweka mkazo katika kuunganisha wabunifu na wawekezaji kupitia majadiliano ya moja kwa moja yaliyolenga kutatua changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa miradi ya tabianchi. Kupitia mikutano hiyo, wabunifu walipata fursa ya kuchunguza uwekezaji na ushirikiano utakaosaidia kukuza miradi yao na kuongeza athari katika jamii.
Akizungumza katika tukio hilo, Elizabeth Richard, Meneja jamii kutoka SmartLab, alisema maonyesho hayo yamekuwa daraja muhimu la kuunganisha wabunifu na wawekezaji, akisisitiza kuwa hatua hiyo imehamisha mjadala kutoka mawazo kwenda kwenye utekelezaji na ukuaji wa miradi. alisema wabunifu wa Tanzania wako tayari kutoa suluhisho zenye matokeo halisi na zinazokidhi mahitaji ya jamii.
“Maonyesho haya yamekuwa daraja muhimu na ni mwanzo au mwendelezo wa kuhamisha mjadala kutoka hatua ya mawazo kwenda katika utekelezaji na ukuaji wa miradi. Hivyo yaliyojadili na kufikia maazimio yanapaswa kuwa mwanzo wa utekelezaji wa miradi.”
Kwa upande wake, Inés Mas de la Peña, Meneja wa Programu wa Climate KIC, alisema mjadala wa jopo uliowakutanisha wataalamu akiwemo Happy Itros kutoka ActionAid, Dk Gerald Kafuku kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech), Ramla Msuya kutoka Benki ya CRDB na Shamim Wasii Nyanda kutoka Hatch Blue ulisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wabunifu, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo ili kuziba pengo la ufadhili. Wataalamu hao walikubaliana kuwa ubunifu pekee hautoshi bila mifumo thabiti ya usaidizi na uwekezaji.