
Unguja. Waziri wa Fedha Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar amesisitiza ushirikiano wa idara za forodha za Afrika ili kufanikisha malengo ya kukusanya mapato kutokana na biashara za kimataifa, kufanikisha biashara na uwekezaji katika mataifa hayo na kupata takwimu za biashara kimataifa.
Balozi Omar ametoa kauli hiyo leo Mei 14, 2026 wakati akifungua mkutano wa Baraza la Uongozi wa Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) unaofanyika Unguja Zanzibar.
Amesema forodha duniani inapita kwenye kipindi kigumu kwa sababu ya ushindani uliopo hivyo unaathiri nchi zote.
“Kwa hiyo tunaposhirikiana tunazifanya idara zetu za forodha kuwa za kisasa kusaidia katika kipindi hiki kigumu,” amesema Balozi Omar.
Amesema kuwa na mfumo mmoja ni sehemu ya kufanikisha biashara na uwekezaji kwa sababu kumekuwapo na mifumo mbalimbali katika idara za forodha lakini ilikuwa ya ndani zaidi katika mamlaka za mapato.
Amefafanua katika miaka ya hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia idara ya forodha, imeanzisha mfumo maalumu unaounganisha taasisi zote zinazohusika na masuala ya forodha zikiwemo binafsi na za Serikali na mamlaka za bandari na zinazosimamia viwango na zinazohusika na uingizaji na uondoaji mizigo bandarini.
Waziri Omar amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kufanya maboresho kwani idara za forodha ndio mlango wa uingizaji wa bidhaa ambazo zinahitajika kwa matumizi ya wananchi na uingizaji wa uwekezaji na mambo mengine na kuunganisha na mataifa mengine.
“Idara ya forodha inaweza ikawa ni kikwazo cha biashara lakini ikawa wafanikishaji wa biashara, kwa hiyo tutaendelea kuwekeza kwenye mifumo na uwezo wa wafanyakazi,” amesema
“Linapokuja suala la sera ya forodha moja inahusu biashara ya ndani na maendeleo ya ukanda na dunia nzima,” amesema.
Naye Kamishana Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema mkutano huo unalenga kuwezesha biashara ambapo wataongeza walipa kodi na mapato na yatasaidia kuendeleza nchi na kusaidia biashara za ndani.
“Hii maana yake mizigo isichelewe bandarini itoke kwa haraka, watu waje wafanye shughuli zao na lingine ni kulinda nchi ili iwe salama kama kuna vitu visivyotakiwa visipite na ili haya yafanyike lazima kuwe na ushirikiano na kubadilishana taarifa kati ya hizi nchi” amesema Mwenda
Amesema Tanzania ipo kimkakati kwani ni mlango mkuu wa takribani nchi nane hivyo maazimio yatakayotoka yatasaidia nchi nyingine na watu wa ndani watapata biashara nyingi na kuajiriwa na shughuli za ndani zitaimarika zaidi.
Naye Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani, Ian Saunders amesema hii fursa ya kupitia changamoto zinazowakabili jumuiya ya forodha, na majibu kwa changamoto hizo kwa njia ya viwango, mwongozo na msaada wa utekelezaji.
“Kuhakikisha tunakua na mtazamo wa pamoja katika kushughulikia changamoto hizi ambazo mara nyingi zinahitaji kujitolea kwa mamlaka za forodha kila moja, lakini pia mtazamo wa kimtandao unaojengwa juu ya kuaminiana na ushirikiano wa taarifa, ili kuhakikisha wale wanaotaka kutumia vibaya mfumo wanazuiwa kwa kila njia iwezekanavyo,” amesema katibu mkuu huyo.
Naye Naibu Kamishna wa Forodha nchini Kenya, David Ontweka amesema wanatarajia Afrika Mashariki kupitia mifumo ya kidijitali kuunganisha biashara ili kukuza biashara, kwenda kutafuta njia za kufanya biashara kidunia.