Dodoma. Stanbic Bank Tanzania imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Sh18 milioni kwa hospitali tatu za umma mkoani Dodoma katika hatua inayolenga kusaidia kupunguza uhaba wa vifaa muhimu vya matibabu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Hospitali zilizonufaika na msaada huo ni Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa ambazo hupokea maelfu ya wagonjwa kutoka Dodoma na mikoa mingine ya Tanzania.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na shuka 300 za hospitali, glovu 150 za upasuaji, sindano 450 na paketi 90 za upasuaji, huku vikitarajiwa kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vifaa vinavyotumika kila siku katika huduma za tiba.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Meneja wa Tawi la Stanbic Bank Dodoma, Joan Mbise amesema msaada huo umetolewa kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya.

Amesema vifaa hivyo vitaongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma kwa wakati na kusaidia wahudumu wa afya kufanya kazi katika mazingira salama zaidi.

“Vifaa hivi vinaweza kuonekana vya kawaida, lakini vina mchango mkubwa katika huduma za kila siku hospitalini. Kila glovu, sindano au shuka lina nafasi katika kulinda maisha ya wagonjwa na kusaidia utoaji wa huduma bora,” amesema Joan.

Kwa mujibu wa benki hiyo, msaada huo ni sehemu ya uwekezaji wa kijamii unaolenga sekta za afya, elimu, elimu ya fedha na mazingira.

Joan amesema Stanbic imeendelea kushiriki katika miradi mbalimbali ya afya nchini ikiwemo kusaidia taasisi na hospitali zinazohudumia wananchi katika maeneo tofauti ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *