
Unguja. Wakati Wizara ya Kazi na Uwekezaji ikikadiria kutumia Sh27.091 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27, imepanga kutekeleza programu 24 kupitia idara zake mbili za uwekezaji, kazi na ajira.
Kupitia programu ya uwekezaji inatarajia kutekeleza mambo makuu manane, zaidi yakijikita katika ushirikiano wa sekta binafsi (PPP).
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti hiyo leo Alhamisi, Mei 14, 2026, katika mkutano wa bajeti wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema kati ya fedha hizo, Sh6.8 bilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara, Sh5.2 bilioni zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, na Sh15 bilioni zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema katika kuimarisha uwekezaji, watafanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo ya PPP ili iendane na mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya Zanzibar kiuchumi, kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar, kuimarisha utekelezaji wa miradi ya PPP iliyopo na kuvutia wawekezaji zaidi.
“Kuratibu uwekezaji wa miradi ya umma inayotekelezwa kwa mfumo wa PPP inayoanzishwa na sekta binafsi kwa kuzingatia mitaji, teknolojia, ubunifu na njia mpya za utekelezaji,” amesema Shariff.
Pia, Shariff amesema wataanzisha kanzi data ya upembuzi yakinifu kwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa na inayotekelezwa kwa mfumo wa PPP kwa lengo la kuhifadhi na kuratibu taarifa zote sehemu moja ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa.
Programu nyingine ni kuendelea kuwajengea uwezo wa kitaalamu watendaji wa Serikali kupitia wizara, idara na taasisi kuandaa miradi ya umma itakayotekelezwa kwa mfumo wa PPP kwa lengo la kuhakikisha uwazi, ufanisi na kulinda maslahi ya Serikali, wawekezaji na wananchi.
Kadhalika wataandaa na kushiriki semina na warsha za PPP na mikutano ya majadiliano na wadau kutoka sekta binafsi, sekta za umma, wafadhili na taasisi za kifedha na wananchi kwa ujumla ili kuongeza uelewa na kuondoa hofu na upotoshaji wa taarifa za uwekezaji kupitia miradi ya umma inayotekelezwa kwa mfumo wa PPP.
Idara ya kazi na ajira
Kwa upande wa kazi, Shariff amesema watathibitisha mikataba ya kazi 12,000 ya wafanyakazi wa ndani na wa nje ya nchi kwa lengo la kuhakikisha mikataba hiyo inakidhi viwango vya kazi kimataifa.
Pia, wataendelea na hatua za kuridhia mikataba sita ya Shirika la Kazi Duniani inayohusiana na hifadhi ya jamii, wafanyakazi wa majumbani, usalama na afya kazini, mafao ya wafanyakazi wanaopata majanga.
Jambo lingine ni kupambana na ajira za watoto katika sehemu za kazi kwa ajili ya kuzuia utumikishwaji wa watoto chini ya miaka 18 na kukamilisha sheria za kazi ili ziendane na mabadiliko ya wakati uliopo, hali ya uchumi pamoja na kulinda maslahi ya wafanyakazi na waajiri.
Wizara hiyo imesema itasimamia sheria ya usalama na afya kazini na kuandaa kanuni saba zinazohusiana na masuala ya usalama na afya kazini na kutoa elimu kwa waajiri, waajiriwa na jamii katika masuala ya kazi ili kuongeza uelewa wa sheria za kazi, miongozo pamoja na haki na wajibu katika maeneo ya kazi.
“Kuendelea na mfumo wa usimamizi wa taarifa za kazi kidijitali ili kuimarisha taarifa za kazi,” amesema waziri huyo.
Maoni ya kamati
Akisoma maoni ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi na Uwekezaji ya Baraza la Wawakilishi, Makame Mohamed Sufiani, amesema wamebaini mwendo wa upatikanaji wa fedha ni mdogo, hivyo kufanya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kushindwa kutimiza malengo yake.
“Tunaishauri Serikali ihakikishe kwa kipindi kilichobaki itoe fedha zinazotakiwa ili kuiwezesha wizara kutimiza malengo yake,” amesema.
Kamati imeshauri wizara kuwa na ushirikiano na Wizara ya Vijana na Uwezeshaji ili kuweka mikakati ya pamoja kuwaunganisha wazanzibari na fursa za ajira nje ya nchi na kuweka mfumo madhubuti wa kukusanya mapato yanayotokana na ajira za wanaofanya kazi nje ya nchi.