Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya watu kuwatumia mabaunsa katika operesheni zinazohusisha ulinzi, ukamataji na uhamishaji wa watu, Serikali imesema kundi hilo halina uhalali wa kisheria kufanya kazi hizo nchini.
Kwa mujibu wa Serikali, mabaunsa ni kama wanamitindo, watunisha misuli na wanatumika kama pambo kwenye matukio ya sherehe na sanaa, lakini si shughuli za ulinzi kwa kuwa, hawana mafunzo ya kazi hiyo.
Hata hivyo, mabaunsa wenyewe wanasema wengi wao wamesomea shughuli za ulinzi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na hawakuwahi kwenda kuifanya kazi hiyo bila kuitwa na watu wanaotambulika kisheria.
Mjadala huo unaibuka wakati ambao, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya mabaunsa kutumika katika shughuli za ulinzi, ukamataji na uhamishaji watu, hadi kusababisha vifo na kujeruhi raia.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Mei 6, 2026 watu waliotajwa kuwa ni mabaunsa waliibua vurugu baada ya kuvunja nyumba za wakazi wa Lupaso, Kibaha mkoani Pwani na kusababisha vifo vya watu watatu, huku 15 wakijeruhiwa.
Kiini cha mashambulizi hayo ni mgogoro wa ardhi kati ya wakazi hao na mtu anayedai kulimiliki eneo hilo na ndiye anayedaiwa kuwatuma mabaunsa hao kuvunja nyumba za wananchi.
Tukio linalofanana na hilo, limetokea pia mkoani Mwanza, mabaunsa wanadaiwa kumshambulia hadi kufariki dunia, kijana aliyefahamika kwa jina la Mzafaru Yunus.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, kijana huyo alishambuliwa akiwa baa baada ya kudaiwa kushindwa kulipa bili ya vinywaji alivyokunywa yenye thamani ya Sh8,000.
Inadaiwa kuwa, alishambuliwa kwa ngumi, mateke, vipande vya mbao na bomba la chuma.
Pia, tukio la mabaunsa kutumika kama walinzi na wahamishaji watu, lilitokea Kinondoni, jijini Dar es Salaam; walitoa vitu vyote vya mjane kutoka ndani ya nyumba, wakitaka kumhamisha kutoka katika nyumba aliyokuwa anaishi kwa nguvu.
Kutokana na matukio hayo, Mei 6, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alipiga marufuku mabaunsa kutumiwa kuwakamata au kuwashikilia raia wanaotuhumiwa kutenda makosa, akieleza kuwa, watu hao hawana taaluma wala mafunzo ya kazi hiyo.
“Jeshi la Polisi tayari nimeshazungumza nalo kwa kina kuhusu suala la mabaunsa. Kuna maeneo tunaelewana na mengine hatuelewani, lakini nataka tutoe funzo kubwa. Ikiwezekana kabla mwezi huu haujaisha, kusiwepo mahali popote ambako mtu anajitokeza kufanya kazi ya polisi au chombo cha dola bila mafunzo rasmi,” alisema Chalamila.
Wadau wanasemaje
Akizungumzia hilo, aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Jamal Rwambow amesema anatambua kuwepo kwa mabaunsa, lakini hakuna sheria inayowatambua rasmi.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
“Watu wanaotambulika ni madalali wa Mahakama ambao majukumu yao huwa yanatambulika kisheria na hata katika kutekeleza majukumu yao wanapaswa kuzingatia taratibu zilizowekwa,” amesema.
Rwambow amesema mara nyingi madalali wanapotekeleza majukumu yanayohitaji matumizi ya nguvu, hulazimika kulijulisha Jeshi la Polisi ili kutoa usimamizi wa shughuli hizo.
“Kadiri muda unavyoenda sheria inakiukwa, shughuli zinazopaswa kufanywa na madalali zinatekelezwa na mabaunsa ambao wanatumia ubabe unaolalamikiwa na wananchi wengi,” amesema.
Amesema mabaunsa mara nyingi huwakamata watu kwa nguvu bila kufuata utaratibu unaotakiwa. Aidha, amesisitiza madalali wa Mahakama wanapaswa kufanya kazi zao bila kutumia kivuli cha watu wasiotambulika kisheria.
Amefafanua kuwa, madalali wa Mahakama ni wale walioteuliwa kwa mujibu wa Kanuni ya 4(a), (b) na 12(4) ya Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama za mwaka 2017.
“Kuna watu wanaotambulika kisheria kufanya shughuli hiyo na wanajulikana kupitia kampuni zao. Hawawezi kwenda kumtoa mtu kwenye nyumba isipokuwa kuna oda ya Mahakama,” amesema.
Wanaowatumia mabaunsa
Dalali anayetambulika na Mahakama wa Kampuni ya Haperi Investment Limited ya Njombe, Happifania Ngonyani, amesema mara nyingi wanapotekeleza kazi zao huomba ulinzi kutoka Jeshi la Polisi.
“Polisi wanakubali kukupatia ulinzi kwenye suala ambalo Mahakama imetoa amri, ingawa kuna shughuli nyingine zilizopo nje ya Mahakama tunashirikiana na mgambo,” amesema Ngonyani.
Amesema urahisi wa kuwapata na gharama ndogo za kuwalipa ndiyo sababu inayowafanya mabaunsa kuendelea kutumika kwa wingi tofauti na madalali wanaotambulika, ambao hulazimika kufuata taratibu maalumu za kisheria.
“Dalali anayetambulika malipo yake yana kiwango kinachotambulika kisheria. Si wote wanaoweza kumudu kiwango hicho ndiyo maana wengine hutumia mabaunsa,” amesema.
Amesema madalali wengi huwa na majukumu mbalimbali ikiwamo udalali wa mahakama, ardhi, nyumba na makazi pamoja na ukusanyaji wa madeni kwa watu binafsi na taasisi.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Kwa mujibu wake, baada ya makubaliano kufikiwa, dalali huweka masharti ya malipo pamoja na gharama nyingine za uendeshaji kama usafiri na malazi.
“Mfano niko Njombe mjini lakini unatakiwa kwenda kumdai mtu aliyeko Ludewa, inanilazimu kumuandikia notisi na wakati mwingine kulala huko siku mbili,” amesema.
Amesema mteja akishakubaliana na masharti hayo, dalali huanza kazi rasmi ya kufuatilia deni.
Pia, amesema kazi yao ina changamoto nyingi na kuiomba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuweka utaratibu wa kuruhusu madalali kushirikiana na polisi hata katika shughuli zisizo na amri ya Mahakama.
Kwa upande wake, Dalali kutoka Kampuni ya T/A Majembe Auction Mart Limited ya Dar es Salaam, Dixon Kitima amesema mabaunsa hutumiwa na madalali kutokana na masharti magumu yanayotolewa na polisi wakati wa kuomba ulinzi.
“Unaweza kuwa na kazi ukaenda kuomba polisi lakini wakakwambia vurugu zikitokea ndiyo uje. Wakati mwingine unaweza kuumizwa kabla hawajafika,” amesema Kitima.
Amesema madalali huwatumia mabaunsa kwa ajili ya kujilinda katika maeneo hatarishi na pia kusaidia kubeba mizigo mizito kutokana na nguvu walizonazo.
“Anayesimamia kazi ya kumtoa mtu ni dalali, lakini kama kuna mzigo mimi siwezi kubeba nitamtafuta baunsa kama kibarua,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Kitima amesema mabaunsa hupatikana kupitia vyama vyao, mahoteli makubwa au kumbi mbalimbali, huku kutumia polisi katika shughuli hizo ikiwa ni nyongeza tu.
“Polisi anatakiwa kusimamia amani lakini wakati mwingine vurugu zikianza anakimbia,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Baa na Kumbi za Starehe Tanzania (Ubakuta), Mponjoli Mwakabana amesema mara nyingi mabaunsa wanaotumika baa wanawatoa kwenye maeneo yao ya mazoezi ‘Gym.’
Pia, amesema wapo mabaunsa wanaoomba kazi kwenye baa na kumbi za starehe na wanapewa.
Amesema hawawatumii mabaunsa kwa ajili ya kulinda watu na vitu tu, bali wanatumika kimkakati kuvutia wateja, sababu mavazi na mionekano yao, inamfanya mteja ajione yuko salama.
“Biashara ya baa ina vivutio vingi. Mtu akiona kuna mabaunsa anaamini kuna ulinzi,” amesema.
Mabaunsa wenyewe wanasemaje
Kiongozi wa Chama cha Mabaunsa (Losa), Andilile Mwaikimba amesema wengi wa wanaofanya kazi hizo wamepata mafunzo mbalimbali ikiwamo kupitia JKT.
“Tunajua namna ya kumkamata mtu na kufanya kazi zetu huwa tunaitwa na madalali,” amesema Mwaikimba.
Amesema wanapopata kazi hupima ukubwa wa shughuli husika kabla ya kupanga gharama, kwa kawaida kila baunsa hulipwa kuanzia Sh40,000.
“Watu wanaohitaji mabaunsa ni wengi na kazi nyingi tunazipata kutoka kwa madalali,” amesema.
Serikali yajibu
Akizungumzia hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema hakuna sheria wala utaratibu wa usajili wa mabaunsa kutekeleza shughuli za ulinzi nchini.
Amesema kumtumia baunsa kutekeleza shughuli za ulinzi na ikiwa hatokani na kampuni ya ulinzi iliyosajiliwa na Serikali ni kosa kisheria.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Mtindo wa mabaunsa, amesema ni kama mfumo mpya ulioibuka na mara nyingi wanatumika kama mapambo au sehemu ya vionjo kwenye matukio ya sherehe na sanaa.
“Kuibuka kwa mfumo huo, si jambo baya na mabaunsa kama mabaunsa hakuna mahali ambako wamesajiliwa. Kinachoweza kusajiliwa ni kampuni ya ulinzi,” amesema.
Mahmoud amesema inapotokea baunsa ametumika kufanya shughuli za ulinzi akamdhuru au kumpiga mtu, anapaswa kuchukuliwa hatua kama mhalifu mwingine.
Amesema Serikali inatambua suala la ulinzi binafsi na kisheria linasimamiwa na Jeshi la Polisi, lililokasimiwa mamlaka ya kusajili kampuni za ulinzi baada ya kujiridhisha nazo.
Naibu waziri huyo amesema kampuni hizo zinazosajiliwa zina walinzi waliofuzu mafunzo ya kuifanya shughuli hiyo na sio mabaunsa.
“Tafsiri ya neno baunsa inapochanganywa na ulinzi ni kosa. Baunsa kiasili ni mwanamitindo, mnyanyua vyuma au mtunisha misuli. Tunapaswa kuondokana na mtazamo wa kuchukua baunsa kumfanya mlinzi,” ameonya naibu waziri huyo.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Amesema mabaunsa hawako rasmi, ingawa kuna utamaduni unaofanya wazoeleke kutumika kama pambo, lakini hakuna utaratibu wa kuwasajili.
“Kwa sasa hakuna utaratibu maalumu wa kuwasaiji mabaunsa kama taasisi ya ulinzi na kama watakuwa na hoja ya kujitengeneza kama taasisi watapaswa kufuata utaratibu,” amesema.
Amewataka mabaunsa kuepuka kuvunja sheria za nchi, kwa sababu kupiga mtu au kumuua ni kujichukulia sheria mkononi, hivyo kwa vyovyote utachukuliwa hatua.