Tanga. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imewakutanisha wanawake wajasiriamali katika Kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu masuala ya ulipaji kodi, kurasimisha biashara zao pamoja na kuwafungua kwenye fursa mbalimbali zinazotokana na kushiriki katika uchumi rasmi.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na wanawake zaidi ya 300 limefanyika Mei 14, 2026 katika jijini Tanga na kuwahusisha wanawake wajasiriamali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Akifungua kongamano hilo, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castrol John amesema wanawake ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa kutokana na ushiriki wao mkubwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema takwimu zinaonesha wanawake nchini wanamiliki asilimia 54 ya biashara ndogo, za kati na za kati ndogo huku ushiriki wao katika nguvu kazi ukikadiriwa kufikia takribani asilimia 80 katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025.
“Ni ukweli usiopingika kwamba bila ushiriki wa wanawake, juhudi za kuongeza wigo wa walipakodi na kuongeza mapato ya ndani haziwezi kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema John.
Amesema TRA imejikita katika kuboresha huduma zake kwa kuzingatia ushirikishaji, uwazi, weledi na urahisi wa upatikanaji wa huduma ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika mfumo wa kodi.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoa wa Tanga akiwa na wadau wengine wa kodi wakiingia kwenye ukumbi wa Jukwaa la Wanawake na TRA jijini Tanga.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, kupitia Jukwaa la Wanawake na Kodi wanawake watapata nafasi ya kupata ushauri wa kodi kwa karibu, kujifunza kuhusu wajibu na fursa zilizopo pamoja na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha huduma za TRA.
“Tunataka mwanamke ajisikie salama, anaheshimiwa, na ashiriki kikamilifu katika mfumo wa kodi bila hofu wala vikwazo visivyo vya lazima,” amesema.
Aidha, amewataka wanawake kutumia jukwaa hilo kujifunza na kuwa mabalozi wa utamaduni wa kulipa kodi katika jamii zao huku akisisitiza kuwa kodi ndiyo injini ya maendeleo inayowezesha utoaji wa huduma za elimu, afya, maji na miundombinu.
“Mwanamke akisimama kiuchumi, familia inaimarika, jamii inakua, na taifa linapiga hatua,” amesema John.
Katika hatua nyingine, amewapongeza wadau wa maendeleo wa Good Financial Governance Programme pamoja na GIZ kwa kuendelea kushirikiana na TRA katika kuhakikisha elimu ya kodi inawafikia wanawake na makundi mbalimbali ya jamii.
Mwakilishi wa Meneja wa Elimu ya Mlipakodi TRA Makao Makuu , Charles Mkumbwa amesema kongamano hilo ni hatua mpya ya kimkakati inayolenga kuwafikia wanawake kwa njia mahsusi ili kuwajengea uelewa sahihi wa masuala ya kodi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi.
Amesema Jukwaa la Wanawake na Kodi lilizinduliwa rasmi Machi 6, 2026 na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, kwa lengo la kutoa nafasi kwa wanawake kujadili kwa uwazi nafasi yao katika uchumi rasmi hususan katika kuelewa ulipaji kodi na fursa zinazotokana na kuwa katika mfumo rasmi wa biashara.
Mkumbwa amesema jukwaa hilo ni daraja la mawasiliano kati ya TRA na wanawake walipakodi pamoja na wale ambao bado hawajaanza kulipa kodi.
Amesema malengo ya jukwaa hilo ni kutoa elimu ya kodi kwa lugha rahisi na inayoeleweka, kusikiliza changamoto za wanawake walipakodi na kuzitafutia ufumbuzi kwa ushirikiano pamoja na kujenga uhusiano wa karibu na kuaminiana kati ya TRA na wanawake waliopo katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
“Jukwaa hili linalenga pia kuwawezesha wanawake kujiunga na mfumo rasmi wa kodi hivyo kupanua wigo wa walipakodi na kuongeza mapato ya Taifa,” amesema Mkumbwa.
Ameeleza kuwa kupitia jukwaa hilo, TRA itaandaa mikutano ya mara kwa mara, mafunzo, kliniki za kodi pamoja na vipindi maalumu vya mawasiliano vitakavyotoa ufafanuzi kuhusu sheria na taratibu za kodi.
Aidha, amesema wanawake wengi bado wapo katika sekta isiyo rasmi, hivyo kupitia Dawati la Uwezeshaji Biashara watasaidiwa kusajili biashara zao, kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kuelewa wajibu wao wa kikodi bila hofu.
Mkumbwa amesema TRA itaendelea kutumia njia mbalimbali za utoaji elimu ya kodi ikiwemo semina, mikutano, vipindi vya redio na televisheni pamoja na elimu ya kodi mlango kwa mlango ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kodi.
“Jukwaa hili si tukio la siku moja, bali ni mwanzo wa safari endelevu ya kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari, uwazi na ushirikiano,” amesema Mkumbwa.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Tanga, Aziza Ramadhan amesema kongamano hilo limefungua ukurasa mpya kwa wanawake wajasiriamali kwa kuwapa nafasi ya kujifunza masuala muhimu ya kodi na namna ya kuendesha biashara zao kwa kufuata taratibu rasmi.
Amesema wanawake wengi wamekuwa wakikosa taarifa sahihi kuhusu kodi jambo ambalo limekuwa likiwafanya baadhi yao kushindwa kupanua biashara zao kutokana na hofu au kutokuelewa wajibu wao wa kisheria.
“Tunaiomba TRA kuendelea kuandaa makongamano haya mara kwa mara kwa sababu yanawajengea wanawake uelewa, kujiamini na kuwafanya washiriki kikamilifu katika uchumi rasmi,” amesema Aziza Ramadhan.
Naye mjasiriamali wa vitafunwa na Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Mwajuma Said amesema kupitia kongamano hilo amepata uelewa mkubwa kuhusu matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na umuhimu wake katika kuendesha biashara kwa kufuata taratibu rasmi.
Amesema elimu hiyo imewasaidia wanawake wengi kuelewa kuwa mfumo wa kodi si wa kuwaogopesha bali ni sehemu ya kukuza biashara zao na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi.
“Awali, nilikuwa sielewi vizuri matumizi ya TIN lakini kupitia elimu hii nimefahamu umuhimu wake katika biashara na nitakuwa balozi kwa wanawake wengine,” amesema Mwajuma Said.
Aidha, amesema wanawake wanapaswa kutumia jukwaa hilo kujifunza zaidi kuhusu masuala ya biashara, sheria za kodi na namna ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa kupitia taasisi za Serikali na sekta binafsi.