Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia katika ushirikiano wa kimkakati wa kifedha wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 40 na taasisi ya British International Investment (BII) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa biashara ndogo na za kati nchini Tanzania. Makubaliano hayo yametangazwa pembezoni mwa mkutano wa Africa CEO Forum 2026 unaofanyika jijini Kigali – Rwanda.

Ushirikiano huo unahusisha utoaji wa ufadhili wa muda mrefu wa dola milioni 15 za Marekani kwa kipindi cha miaka mitano, ukiwa na lengo la kusaidia ukuaji wa biashara, kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa Kitanzania na kuimarisha uthabiti wa uchumi. Kupitia mpango huo, wafanyabiashara watanufaika na mitaji ya kuendesha biashara, huduma za kifedha za ndani na nje ya nchi pamoja na suluhisho bunifu zitakazowasaidia kupanua shughuli zao.

Waziri wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji, ubunifu na ushindani wa biashara za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa. Takwimu zinaonesha kuwa biashara ndogo na za kati zinachangia zaidi ya asilimia 90 ya biashara zote nchini pamoja na kutoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi amesema ushirikiano huo unaashiria kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa katika sekta binafsi ya Tanzania pamoja na mchango wa taasisi za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.

Mkurugenzi Mkuu na Mkuu wa Kanda ya Afrika wa BII, Chris Chijiutomi amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya BII katika kusaidia biashara ambazo bado zinakabiliwa na changamoto ya kupata huduma za kifedha, akibainisha kuwa mpango huo utasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi, ubunifu na ajira nchini Tanzania.

#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *