
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), Mohammad-Baqer Qalibaf, ameonya kuwa juhudi za Marekani za kuendeleza mvutano wa kijeshi karibu na Mlango wa Hormuz zinaweza kusababisha mgogoro mpya wa kifedha duniani, wakati ambapo deni la taifa la Marekani tayari limefikia kiwango kikubwa cha dola trilioni 39.
Qalibaf alitoa kauli hizo katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X siku ya Alhamisi, baada ya taarifa kuonyesha kuwa faida ya hati fungani za Hazina ya Marekani za miaka 30 imepanda zaidi ya asilimia tano kwa mara ya kwanza tangu kabla ya mgogoro wa kifedha wa dunia wa mwaka 2008, huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu mfumuko wa bei na gharama za nishati zinazochochewa na vita. Wakati faida ya hati fungani inapopanda hadi viwango vya juu kiasi hiki, kwa kawaida humaanisha kuwa wawekezaji wanahitaji fidia kubwa zaidi kutokana na hofu ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kuongezeka kwa deni la serikali, au viwango vya juu vya riba kuendelea kwa muda mrefu zaidi.
Qalibaf ameandika kuwa: “Kwa hiyo mnamfadhili [Pete] Hegseth, mtangazaji wa televisheni aliyeshindwa, kwa viwango vya riba ambavyo havijashuhudiwa tangu 2007, ili aje kuigiza kama Waziri wa Vita katika eneo letu la Hormuz?” Qalibaf aliandika, akirejelea taaluma ya zamani ya waziri huyo wa vita Marekani katika televisheni.
Mnamo Aprili 13, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuendelea mzingiro haramu dhidi ya meli na bandari za Iran, hatua iliyokiuka masharti ya usitishaji vita aliyokuwa ametangaza mapema mwezi huo.
Iran, ambayo tayari ilikuwa imeufunga Mlango wa Hormuz kwa maadui wake na washirika wao kujibu uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya nchi hiyo kati ya Februari 28 na Aprili 7, baadaye ilianza kuweka udhibiti mkali zaidi katika njia hiyo ya kimkakati ya bahari.
Jamhuri ya Kiislamu imekataa kurejea katika mazungumzo na Washington hadi pale matakwa ya Tehran yatakapotekelezwa, yakiwemo kuondolewa kwa mzingiro huo, kuhakikisha mwisho kamili wa aina yoyote ya vita katika nyanja zote, pamoja na kutolewa kwa fidia ya hasara iliyopatikana vitani..
Hegseth na Trump wamekuwa wakitoa taswira ya ushindi kuhusu vita hivyo na pia kuhusu msimamo wa sasa wa Marekani dhidi ya Iran.
Hata hivyo, ripoti nyingi zimekuwa zikionesha hali tofauti, ikiwemo zile zinazobaini kuwa waziri huyo wa vita wa Marekani alimpa Trump taarifa za kupotosha kuhusu kile kilichodaiwa kuwa “mafanikio ya Marekani” dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.