Wizara ya Maliasili na Utalii, imepanga kutumia Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico kuanzia mwezi ujao, kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.

Hayo yameainishwa katika bajeti ya wizara hiyo inayosomwa leo bungeni Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji.

Uamuzi wa kutumia Fainali za Kombe la Dunia 2026 kutangaza Utalii, ni muendelezo wa hatua za Serikali kutumia ushawishi wa soka kuvutia kundi kubwa la watu kutoka maeneo mbalimbali.

Waziri Kijaji ameainisha kwamba Tanzania itaandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda hivyo kabla ya kutumia mashindano hayo kujitangaza kimataifa, itaanzia katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

“Kwa kuwa Tanzania ni moja ya waandaaji wa mashindano hayo, wizara imeandaa mkakati wa kuitangaza Tanzania kama kivutio cha kipekee cha utalii.

“Mkakati huo unahusisha shughuli za kabla, wakati na baada ya mashindano ambapo kabla ya mashindano hayo, shughuli zinazotarajiwa

kutekelezwa ni pamoja na kuanza kutangaza utalii wa Tanzania wakati wa Mashindano ya Dunia ya Mpira wa Miguu yaani FIFA World Cup yatakayofanyika nchini Marekani kati ya mwezi Juni na Julai mwaka 2026.

“Kupitia mashindano hayo Tanzania itashirikisha wadau muhimu

wakiwemo watangazaji mashuhuri wa michezo duniani na kujitangaza kupitia mabango ya kidijitali “billboards” yatakayowekwa katika maeneo ya kimkakati nchini Marekani,” amesema Waziri Kijaji.

Waziri Kijaji ameanika kuwa katika kuhakikisha kunakuwa na urahisi kwa wageni watakaokuja nchini katika fainali za AFCON, Serikali imepanga kutumia reli ya SGR kuufungua utalii wa Mkoa wa Morogoro hasa Hifadhi ya Wanyama ya Mikumi.

“Wizara itaunganisha Hifadhi ya Taifa Mikumi na reli ya SGR kupitia ujenzi wa lango la kuingia wageni katika eneo la Kilosa. Hatua hiyo itarahisisha wageni watakaokuja jijini Dar es Salaam kushiriki AFCON waweze kusafiri na reli kwenda kutalii Mikumi.

“Vilevile, Wizara imekamilisha ujenzi wa uwanja wa gofu wenye hadhi ya Kimataifa katika Ikolojia ya Serengeti ili kuvutia watalii wa michezo hususan watakaotembelea Tanzania kipindi cha mashindano ya AFCON 2027,” amesema Waziri Kijaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *