Bodi mpya Moruwasa yapewa zigo la ubora wa majiBodi mpya Moruwasa yapewa zigo la ubora wa maji

Morogoro.  Bodi mpya ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (Moruwasa) imeelekezwa kusimamia kwa karibu ubora wa miradi ya maji ili kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaleta tija kwa wananchi na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji mkoani Morogoro.

Uteuzi wa bodi hiyo ya 10 umefanyika Mei 15, kufuatia ile iliyokuwa madarakani kumaliza muda wake, na Serikali imeitaka kuwa na usimamizi madhubuti ili kuepusha matumizi makubwa ya fedha yasiyoendana na matokeo kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema miradi ya maji inahitaji usimamizi makini ili kuhakikisha inaleta manufaa yaliyokusudiwa.

Amesema bila usimamizi thabiti, kuna hatari ya kutumia gharama kubwa katika miradi lakini mwisho wake isiweze kuwasaidia wananchi kama ilivyokusudiwa.

“Niiombe bodi hii, pamoja na majukumu mengine, msimamie kwa karibu menejimenti ya Moruwasa katika miradi ya maji, iwe inatekelezwa na wakandarasi au kupitia force account (Serikali inatumia wataalamu, vifaa na wafanyakazi wake yenyewe),” amesema Waziri.

Ameongeza kuwa bodi inapaswa kuhakikisha rasilimali za mamlaka hiyo zinasimamiwa kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na ufanisi, sambamba na kuhakikisha hesabu zinakaguliwa kwa wakati ili kupata hati safi.

Katibu Mkuu amesema Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana nayo pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira inaimarika kulingana na ukuaji wa Mkoa wa Morogoro na mahitaji ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Moruwasa, Sais Kyejo amesema bodi iliyomaliza muda wake imefanya kazi nzuri na kuweka msingi wa maboresho ya huduma za maji.

Amesema baadhi ya maeneo kama Mkundi na Lukobe yameendelea kunufaika na miradi ya maji inayotekelezwa na mamlaka hiyo, huku akiahidi kushirikiana na bodi mpya kukamilisha miradi mingine inayoendelea.

Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Profesa Moses Warioba ameiomba menejimenti ya Moruwasa, watumishi na wadau wote kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya zamani na mipya.

Amesema bodi hiyo itaweka kipaumbele katika kuhakikisha changamoto ya maji inatatuliwa kwa ufanisi.

Awali akizindua bodi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ameitaka bodi mpya kuhakikisha inashughulikia changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *