Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote, katika Ikulu ya Dar es Salaam, wakati mjadala ukiendelea Afrika Mashariki kuhusu nchi itakayojengwa kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta ghafi.
Ingawa Ikulu haijatoa maelezo rasmi ya mazungumzo hayo hadi saa 7:00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki, picha zilizotolewa zinaonesha wawili hao katika mazungumzo.
Ziara ya Dangote inakuja katika kipindi ambacho kuna mjadala kuhusu eneo la kujengwa kwa mradi wa kiwanda cha mafuta unaokadiriwa kuwa na thamani ya Dola bilioni 15 hadi 17 za Marekani, na uwezo wa kuchakata mapipa 650,000 kwa siku.
Mjadala huo ulizidi kuchukua sura mpya baada ya Rais wa Kenya, William Ruto, kudokeza jijini Nairobi kuwa mradi huo unaweza kujengwa Tanga, Tanzania, akitaja bandari ya mji huo kuwa na nafasi ya kimkakati katika kukuza ushirikiano wa kikanda.
Hata hivyo, Ruto alisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu eneo la mradi huo utabaki mikononi mwa wawekezaji binafsi wanaoongozwa na Dangote.
Katika muktadha mwingine, Dangote alinukuliwa na gazeti la Financial Times akisema anaelekea kupendelea Mombasa, Kenya, akitaja bandari ya kina kirefu, miundombinu imara ya usafirishaji na ongezeko la mahitaji ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza usalama wa nishati katika kanda hiyo na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati, huku ukihudumia masoko ya Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine jirani.
Wakati huohuo, Tanzania na Uganda zinaendelea kukamilisha ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga.
Uganda inatarajiwa kuzalisha takribani mapipa 230,000 ya mafuta kwa siku mara uzalishaji wa kibiashara utakapoanza, huku mradi wa EACOP ukimilikiwa kwa hisa na TotalEnergies (asilimia 62), TPDC na UNOC (asilimia 15 kila mmoja), na China National Offshore Oil Corporation (asilimia 8).
