Iran: Walioanzisha vita wanabeba dhima ya hali ya sasa ya Hormuz na athari zake mbaya za kiuchumiIran: Walioanzisha vita wanabeba dhima ya hali ya sasa ya Hormuz na athari zake mbaya za kiuchumi

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York amesema kuwa walioanzisha vita dhidi ya Iran na washirika wao katika kanda hii wanabeba dhima kamili ya hali ya sasa katika Mlango-Bahari wa Hormuz na athari zake mbaya za kiuchumi duniani.

Akizungumza Ijumaa katika kikao maalumu cha Mkutano Maalumu wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC) uliopewa jina la “Kulinda Mitiririko ya Nishati na Ugavi” Amir Saeid Iravani ametahadharisha kuhusu kuendelea kuyumba masoko ya nishati, minyororo ya usambazaji na mtiririko wa biashara duniani.

Iravani amesema, katika muktadha huu, Iran imeteseka kwa njia mbili kubwa na zenye mfungamano na kwamba katika muda wa chini ya mwaka mmoja Iran imekabiliwa mara mbili na mashambulizi haramu ambayo ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Mwakilishiwa Kudumu wa Iran UN amesema mashambulizi hayo yameua maelfu ya raia wasio na hatia hususan wanawake na watoto na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya kiraia, kiuchumi, nishati na mazingira.

Ameongeza kuwa: Ukosefu wa utulivu wa sasa haukutokea katika ombwe. Umesababishwa na kuongezeka kwa hatua za kijeshi na mashambulizi yaliyo kinyume cha sheria ya utawala wa Israel na Marekani.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alihitimisha hotuba yake kwa kusema: Tunatangaza wazi kwamba waanzilishi wa vita dhidi ya Iran na washirika wao wa kikanda wanabeba dhima ya hali ya sasa katika Mango-Bahari wa Hormuz na athari zake mbaya za kiuchumi duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *