Dar es Salaam. Mpango wa Tanzania kuingia kwenye uwekezaji mkubwa wa kusafisha mafuta ghafi umeanza kupata sura mpya baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaji Aliko Dangote, kuhusu uwezekano wa kutekeleza mradi mkubwa wa kiwanda cha mafuta unaokadiriwa kugharimu Dola bilioni 17 za Marekani
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Dar es Salaam leo, Mei 16, 2026, yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa Serikali na kampuni za Dangote katika sekta za nishati, viwanda, bandari, gesi, mbolea na miundombinu.
Kwa mujibu wa Dangote, mradi huo wa kusafisha mafuta ghafi unatarajiwa kuwa wa kimkakati kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Ethiopia, huku ukifungua fursa kwa nchi nyingine kushiriki kupitia mfumo wa umiliki wa hisa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na mfanyabiashara kutoka nchini Nigeria ambaye pia ni mwanzilishi na mmiliki wa Dangote Group, Aliko Dangote, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la mradi huo ni kusaidia bara la Afrika kujitosheleza katika uzalishaji wa mafuta na bidhaa zake, sambamba na kupunguza utegemezi wa kuagiza mafuta kutoka nje ya bara.
“Mradi huu utasaidia nchi za Afrika Mashariki kupata usalama wa nishati na kujilinda dhidi ya misukosuko ya bei na changamoto za upatikanaji wa mafuta duniani,” amesema Dangote.
Mfanyabiashara huyo pia ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, akisema hatua zilizochukuliwa na Serikali kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara zimeongeza ufanisi wa shughuli za kampuni hiyo nchini.
“Nataka nikushukuru kwa dhati kwa kushughulikia changamoto nyingi za uwekezaji wetu wa kiwanda cha saruji Mtwara. Ulipoingia madarakani tulikuwa na changamoto nyingi, lakini kama ulivyoahidi, kila changamoto imeshughulikiwa ipasavyo,” amesema Dangote.
Amesema kutokana na maboresho hayo, kampuni yake imeendelea kuiona Tanzania kama eneo muhimu la uwekezaji barani Afrika.
Katika hatua nyingine, Dangote amesema kampuni yake tayari imeingiza nchini malori 400 yanayotumia gesi asilia kwa ajili ya kusafirisha na kusambaza saruji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kampuni kubadilisha malori 700 kutumia nishati mbadala kwa lengo la kuongeza ufanisi wa shughuli zake na kupunguza gharama za uendeshaji.
Amesema matumizi ya gesi asilia katika usafirishaji yatasaidia kupunguza matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji wa biashara, sambamba na kuunga mkono juhudi za matumizi ya nishati safi.
Akizungumzia uzalishaji wa kiwanda cha saruji cha kampuni hiyo, amesema a kinaendelea kufanya vizuri na kinatarajia kuzalisha tani milioni 2.8 mwaka huu, karibu kufikia lengo la tani milioni 3.2.
“Tunaendelea kufanya vizuri, na hilo linatokana na mazingira bora ya biashara yaliyopo chini ya uongozi wa Rais Samia,” amesema Dangote.
Kwa upande wake, Rais Samia amemhakikishia Dangote ushirikiano wa Serikali, huku akimtaka kuendelea kuangalia fursa nyingine za uwekezaji nchini zitakazowanufaisha wawekezaji na Watanzania kwa ujumla.
Pia amemkaribisha kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea, akisema Tanzania bado ina mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo kuliko uwezo wa uzalishaji wa ndani.
