
Dar es Salaam. Katika dunia ya leo, simu janja, televisheni za kisasa, YouTube, TikTok na michezo ya mtandaoni vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watoto wengi.
Mtoto wa miaka kuanzia miwili na nusu, mitatu au minne anaweza kujua namna ya kufungua video kwenye simu kabla hata hajajua kufunga vifungo vya shati lake.
Wazazi wengi wanajikuta wakitumia skrini kama njia ya kumtuliza mtoto, kumfanya ale chakula au kumpunguzia usumbufu.
Taratibu, teknolojia imeanza kushika nafasi ambayo zamani ilijazwa na mazungumzo ya familia, michezo ya nje na ukaribu wa wazazi kwa watoto wao.
Swali kubwa linabaki: Je, watoto wanapata wazazi wapya kupitia skrini?
Ni kweli kwamba teknolojia imeleta manufaa mengi. Mtoto anaweza kujifunza lugha mpya, hesabu, sayansi na hata ubunifu kupitia video na michezo ya kielimu.
Kuna watoto ambao wamepata uwezo mkubwa wa kufikiri na kujiamini kutokana na matumizi sahihi ya teknolojia.
Hata hivyo, pamoja na manufaa hayo, kuna hatari inayoongezeka kimyakimya; watoto wengi wanalelewa zaidi na skrini kuliko na wazazi wao.
Mtoto anayekaa muda mrefu kwenye YouTube au TikTok huanza kujifunza maadili, lugha na mitazamo kutoka kwa watu asiowajua. Wengine huiga mavazi, tabia, misemo na hata mienendo ya watu maarufu mitandaoni bila kuelewa athari zake.
Kinachoumiza zaidi ni kwamba, mara nyingi watoto hawa hawapati muda wa kutosha wa kuongozwa na wazazi wake kuhusu kile wanachokiona.
Katika familia nyingi za sasa, wazazi wako bize kutafuta maisha. Wanarudi nyumbani wakiwa wamechoka, hivyo simu au televisheni inakuwa mlinzi wa mtoto.
Mtoto akilia anapewa simu, akitaka kula anawekewa katuni, akichoka anaruhusiwa kucheza michezo ya mtandaoni kwa saa nyingi. Bila kutambua, mzazi anaachia sehemu ya jukumu lake kwa teknolojia.
Hata hivyo, mtaalamu wa saikolojia ya mtoto, Godfrey Mwakaluswa anasema tatizo si matumizi ya teknolojia pekee, bali ni pale ambapo teknolojia inachukua nafasi ya malezi.
“Malezi si kumpatia mtoto chakula na mavazi pekee. Malezi ni uwepo wa mzazi katika maisha ya mtoto; kusikiliza, kuelekeza, kufundisha maadili na kujenga ukaribu wa kihisia,” anasema Mwakaluswa.
Kwa kauli yake hiyo, ni wazi kuwa inatufumbua macho wazazi kuwa skrini haiwezi kumfundisha mtoto huruma ya kweli, uvumilivu wala namna ya kushughulikia hisia zake. Haya hujengwa kupitia uhusiano wa karibu ndani ya familia.
Hivi karibuni nilizungumza kwa nyakati tofauti na wataalamu wa saikolojia juu ya hoja hiyo, wakaonya kuwa matumizi makubwa ya skrini kwa watoto yanaweza kuathiri uwezo wake wa kuwasiliana vizuri na watu, kuzingatia masomo na hata afya ya akili.
Wanasema watoto wengine hukosa usingizi wa kutosha kutokana na kuangalia video usiku. Wengine hukosa muda wa kucheza na wenzao, jambo linaloweza kuathiri ukuaji wao pia.
Zaidi ya hapo, mitandao kama TikTok imeongeza changamoto mpya. Maudhui mengi huwasilishwa kwa kasi kubwa na kwa mvuto unaoweza kumteka mtoto kirahisi.
Mtoto anaweza kutumia saa nyingi akitazama video fupi bila kuchoka. Kadiri anavyoendelea kuangalia, ndivyo akili yake inavyozoea kupata burudani ya haraka kila wakati.
Hali hii inaweza kupunguza uwezo wa mtoto kuwa na subira au kufanya mambo yanayohitaji umakini wa muda mrefu kama kusoma vitabu.
Hata michezo ya mtandaoni imekuwa na ushawishi mkubwa kwa watoto. Tunaambiwa baadhi ya michezo hujenga ubunifu na uwezo wa kufikiri, lakini mingine huongeza uraibu, hasira au tabia ya kujitenga.
Kuna watoto wanaokasirika wakinyimwa simu kana kwamba wameondolewa sehemu muhimu ya maisha yao. Hiyo ni ishara kwamba teknolojia imeanza kuwatawala badala ya wao kuitawala.
Suluhisho si kupiga marufuku teknolojia kabisa. Bali nianchotaka kushauri hapa ni kuwa, dunia ya sasa haiwezi kutenganishwa na maendeleo ya kidijitali.
Ila kinachohitajika ni wazazi kuwa karibu zaidi na watoto katika matumizi ya teknolojia. Mzazi anapaswa kujua mtoto anaangalia nini, anacheza mchezo gani na anamfuata nani mitandaoni.
Pia, ni muhimu kuweka mipaka ya muda wa kutumia skrini na kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kuzungumza, kusoma, kucheza na kushiriki shughuli za kifamilia.
Nasema hivyo kwa sababu, watoto wanahitaji zaidi uwepo wa wazazi kuliko uwepo wa intaneti. Wanahitaji kusikia sauti za wazazi wao kuliko sauti za watengeneza maudhui mitandaoni.
Wanahitaji kukumbatiwa, kushauriwa na kuelekezwa. Teknolojia inaweza kuwa msaada mzuri katika malezi, lakini isiwe mbadala wa mzazi.
Katika zama hizi za kidijitali, jukumu kubwa la mzazi si kumzuia mtoto kuiona dunia ya teknolojia, bali kuhakikisha teknolojia haichukui nafasi yake moyoni mwa mtoto.
