
Jaji wa Ufaransa atachunguza mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi mwaka 2018 kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu dhidi ya Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.
Mohammed bin Salman na Saudi Arabia walikabiliwa na lawama kubwa za kimataifa baada ya mwandishi habari Jamal Khashoggi kuuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul mnamo 2018. Mashirika ya ujasusi ya Marekani hapo awali yalihitimisha kwamba Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ndiye aliyehusika moja kwa moja na operesheni hiyo ya mauaji.
Khashoggi, aliyekuwa akiishi Marekani na mwandishi wa habari wa gazeti la The Washington Post anayejulikana kwa ukosoaji wake dhidi ya utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, aliuawa na kukatwa vipande vipande ndani ya ubalozi wa Saudi mjini Istanbul.
Malalamiko hayo yaliwasilishwa awali nchini Ufaransa wakati wa ziara ya Mohammed bin Salman nchini humo Julai 2022 na shirika la Khashoggi, Democracy for the Arab World Now (DAWN), na kundi la utetezi wa kisheria la Trial International.
Baadaye shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka, (Reporters Without Borders au RSF kwa kifupi) pia lilijiunga na mashtaka hayo.
“Uhalifu ambao Jamal Khashoggi alikuwa mwathirika wake ni jinai ya kuchukiza, iliyoamuliwa na kupangwa katika ngazi ya juu ya serikali ya Saudi Arabia, ambayo ilipelekea kuuawa mwandishi wa habari aliyekuwa sauti huru ya upinzani,” amesema Emmanuel Daoud, wakili anayewakilisha RSF.
Licha ya tathmini ya taasisi za ujasusi za Marekani kuhitimisha kwamba Mwanamfalme Mohammed bin Salman aliamuru operesheni ya mauaji hayo, Rais Donald Trump alisema wakati alipomkaribisha Bin Salman Ikulu ya White House kwamba “hajui chochote kuhusu suala hilo!”
Mwandishi wa habari wa ABC News alipoibua suala hilo mbele ya vyombo vya habari, Trump alikosoa mtandao huo na kupendekeza leseni yake ifutwe.
