
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen amesema harakati ya muqawama ya nchi hiyo Ansarullah iko “bega kwa bega” na harakati ya mapambano ya Lebanon Hizbullah katika kukukabiliana na njama na uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel.
Abdulwahid Abu Ras alisema haya Ijumaa katika ujumbe wake kwa Ammar al-Moussawi Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Kiarabu na Kimataifa wa Hizbullah.
Amesisitiza kuwa, Lebanon ina ushawishi wa moja kwa moja na mkubwa katika kuunga mkono kadhia ya Palestina na watu wake madhulumu.
Abu Ras aidha ametilia mkazo udharura wa kuwepo mshikamano imara na usioyumba wa serikali ya Sana’a kwa taifa la Lebanon na harakati ya Hizbullah katika mapambano yao dhidi ya utawala wa Tel Aviv.
Hapo awali, kiongozi wa Ansarullah ya Yemen, Abdul-Malik al-Houthi, alionya kwamba Israel haitasitisha hatua zake Asia Magharibi baada ya kushindwa kwa aibu katika vita dhidi ya Iran, akielezea mradi wa Israel kama tishio kubwa kwa wanadamu wote.
Siku ya Ijumaa, Abdul Malik al Houthi alisema kuwa kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu na matukufu ya Kiislamu kunakofanywa na maafisa wa Israel na maajenti wao kunafanyika kwa lengo la kuhujumu Uislamu na Waislamu.
