Velayati aikosoa Marekani kwa vitisho Dhidi ya Iran, aonya inaangukia “mtego” wa IsraelVelayati aikosoa Marekani kwa vitisho Dhidi ya Iran, aonya inaangukia “mtego” wa Israel

Ali Akbar Velayati, mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameonya kuwa Marekani inaangukia “mtego wa kimkakati” uliotegwa na Israel, akisema kuwa Marekani itapoteza kabisa mabaki ya uaminifu wake katika eneo la Asia Magharibi iwapo itaanzisha vita vingine dhidi ya Iran.

Daktari Velayati, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu nchini Iran, ameandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X siku ya Jumapili kwamba “diplomasia tasa” ya Rais wa Marekani Donald Trump huko Beijing na kurejea kwake “bila mafanikio” kutoka China kunaonyesha “mgogoro wa makadirio ya kisiasa” ndani ya utawala wa Washington.

Trump alizuru China mapema wiki hii na kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Xi Jinping kujadili masuala kadhaa, ikiwemo vita dhidi ya Iran na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

Baada ya mkutano huo, rais wa Marekani alisema anafikiria uwezekano wa kuondoa vikwazo vya Marekani dhidi ya makampuni ya mafuta ya China yanayonunua mafuta ya Iran, licha ya vizuizi ambavyo Washington imeviweka dhidi ya Iran.

Xi hakutoa maelezo kuhusu mazungumzo yake na Trump kuhusu Iran, lakini Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilikosoa vita hivyo, ikisema kwamba “havikupaswa kamwe kutokea na havina sababu ya kuendelea.”

Dkt. Velayati pia ametaja hasira ya Abu Dhabi kufuatia taarifa za ziara ya siri ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Umoja wa Falme za Kiarabu, pamoja na “utengenezaji wa taarifa potofu” na Pentagon, kama mifano mingine ya mgogoro wa makadirio unaoikumba Marekani.

Ameandika kwamba, “Katika mazingira kama haya, vitisho vya Trump vinavyochochewa na uchochezi wa Tel Aviv vinamaanisha kuingia katika mtego wa kimkakati.”

Velayati ameonya kuwa kuangukia katika shimo hilo kwa kutumia “kamba ya Israel” kutaleta gharama kubwa, akiongeza kuwa hivi karibuni Washington italazimika kutafuta kwa taa mabaki ya uaminifu wake katika eneo la Asia Magharibi.

Onyo hilo linakuja wakati Trump akiendelea kuongeza matamshi ya vitisho vya vita dhidi ya Iran, karibu miezi mitatu baada ya Marekani na Israel kuanzisha vita vya mashambulizi dhidi ya nchi hiyo vilivyodumu kwa siku arobaini.

Wakati huo huo, bei ya gesi nchini Marekani imepanda kwa kasi na huenda ikaongezeka zaidi huku Iran ikiendelea kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz. Mfumuko wa bei pia unaongezeka kwa haraka, na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu umepita ongezeko la mishahara ya Wamarekani mwezi Aprili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *