
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amefanya mazungumzo ya simu kwa nyakati tofauti na mawaziri wenzake wa Ufaransa, Qatar, Uturuki, na Korea Kusini, siku ya Jumapili, ili kutathmini mahusiano ya pande mbili, matukio ya kieneo na mchakato wa kidiplomasia unaoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa, Araghchi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, wamejadiliana masuala ya nchi mbili na mwelekeo wa kidiplomasia wa sasa.
Aidha Araghchi amefanya mazungumzo ya simu na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, ambapo viongozi hao wawili walibadilishana mawazo kuhusu hali tete ya kanda hii.
Vilevile, siku ya Jumapili jioni, Araghchi alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, wakijadili hatua za kidiplomasia zinazochukuliwa na matukio ya kieneo. Araghchi pia alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Cho Hyun, kuhusu hali ya eneo.
Katika mazungumzo hayo, Araghchi alibainisha hali ya sasa katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, akisisitiza kuwa ukosefu wa usalama unaoikabili kanda hii na madhara yake ya kimataifa, vinatokana na hatua za uchokozi za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwawajibisha wahusika hao kwa ukiukaji huu wa sheria za kimataifa na uhalifu wanaouendeleza.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini amesisitiza msimamo wa nchi yake kuhusu umuhimu wa kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa baharini katika kanda hii na ulimwenguni kote. Aidha, ameonyesha matumaini kuwa juhudi za kidiplomasia zitafikia muafaka haraka iwezekanavyo.
Ikumbukwe kuwa, Iran ilifunga Lango Bahari la Hormuz kwa maadui zake na washirika wao kufuatia kuanza kwa uchokozi usio halali wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu tarehe 28 Februari.
Iran ilianza kutekeleza udhibiti mkali zaidi mwezi uliopita baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kizuizi haramu dhidi ya meli na bandari za Iran, hatua ambayo ni ukiukaji wa masharti ya usitishaji vita uliosimamiwa na Pakistan, ambao ulianza kutekelezwa tarehe 8 Aprili.
Hivi karibuni, Marekani ilianzisha operesheni ya kijeshi iliyodaiwa kulenga kufungua kwa nguvu Lango la Hormuz, lakini ililazimika kusitisha harakati hizo mbele ya msimamo thabiti wa Iran dhidi ya uharamia wa Marekani na vitisho kwa usalama wa baharini.
