Mtwara. Wanafunzi wanaoshiriki majukwaa ya sekta ya mafuta na gesi mkoani Mtwara wameliomba Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwapatia fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu gesi asilia kupitia ziara katika miradi mbalimbali ya gesi.
Wanafunzi hao wanaamini hatua hiyo itawaongezea uelewa kuhusu matumizi na umuhimu wa rasilimali hiyo kwa maendeleo ya taifa.
Ombi hilo limetolewa Mei 18, 2026 wakati maofisa wa TPDC walipotembelea baadhi ya majukwaa ya wanafunzi katika shule za sekondari za Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya programu hiyo pamoja na kutoa elimu kuhusu shughuli za mafuta na gesi asilia.
Wanafunzi walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu uchimbaji, uchakataji na matumizi ya gesi asilia. Wengi wao walionyesha hamu ya kupata uelewa wa kina kuhusu namna sekta hiyo inavyochangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Magamba, Loveness Japhet, alisema majukwaa hayo yamewasaidia kujifunza mambo mengi kuhusu gesi asilia na kuwajengea hamasa ya kutaka kushuhudia kwa karibu shughuli zinazotekelezwa na TPDC.
Mtumishi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kushoto, akitoa zawadi kwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Alisema ziara za mafunzo katika maeneo ya miradi ya gesi zitawasaidia wanafunzi kuelewa kwa urahisi zaidi matumizi ya nishati hiyo katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, usafirishaji na matumizi ya majumbani.
“Tunapata elimu nyingi kupitia majukwaa haya, lakini tukipata nafasi ya kuona miradi kwa vitendo tutapata uelewa mkubwa zaidi na kuongeza hamasa ya kupenda masomo ya sayansi,” alisema Loveness.
Kwa upande wake, mwalimu mlezi wa Jukwaa la Mafuta na Gesi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara, Aurelia Kimaro, alisema wanafunzi wamekuwa wakionyesha shauku kubwa ya kufahamu matumizi ya gesi asilia, hususan katika magari na viwanda.
Alisema sekta ya mafuta na gesi ni pana na inahitaji elimu ya kina ili kuwasaidia wanafunzi kuelewa nafasi ya rasilimali hiyo katika uchumi wa nchi pamoja na fursa zinazopatikana kupitia sekta hiyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii mwandamizi kutoka TPDC, Ali Muluge akizungumza na Wanafunzi ( hawaonekani pichani) ambao wameshiriki kwenye jukwaa la mafuta na Gesi asilia
“Ziara za mafunzo zitawawezesha wanafunzi kuona shughuli za uchakataji na matumizi ya gesi asilia, jambo ambalo litaongeza hamasa ya kujifunza zaidi,” alisema Aurelia.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka TPDC, Ali Muluge alisema shirika hilo linaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi wanaoshiriki majukwaa hayo kwa kuwapatia vifaa vya kujifunzia pamoja na kuwawezesha kutembelea baadhi ya miradi ya mafuta na gesi.
Alisema TPDC imeanzisha majukwaa ya mafuta na gesi katika shule 16 za sekondari mkoani Mtwara kwa lengo la kutoa elimu sahihi kuhusu shughuli za sekta hiyo, hasa katika maeneo ambayo miundombinu ya gesi asilia imepita.
Kwa mujibu wa Ali Muluge, lengo la kuanzishwa kwa majukwaa hayo ni kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na kuwaandaa wataalamu wa baadaye, watakaoshiriki katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini.
