Zuchu anavyotembea na kivuli cha marehemu kaka yakeZuchu anavyotembea na kivuli cha marehemu kaka yake

Dar es Salaam. Machi 2007, tasnia ya muziki wa Taarabu ilipata pigo baada ya kumpoteza mwanamuziki, Omary Kopa, mtoto wa nguli wa muziki wa Mwambao, Khadija Kopa.

Omary Kopa alifariki dunia Machi 26, 2007 akiwa na umri wa miaka 23 na kuzikwa siku iliyofuata visiwani Zanzibar. Licha ya kuondoka akiwa bado kijana, aliacha alama kubwa kupitia nyimbo zake ambazo zinaendelea kuishi hadi leo. Ikiwemo Ee Bwana Ndiyo, Kindumbwe Ndumbwe, Nifagilieni, Imetulia Hiyo, Mambo Hadharani, Kama Noma na Hakuna Kulala.

Mbali na kuacha alama kubwa, mdogo wake ambaye ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Zuchu amekuwa akitumia baadhi ya mistari ya Omary katika nyimbo zake.

Miezi mitatu iliyopita, Zuchu aliachia wimbo wake Bado Nakupenda, ambao hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni nne katika mtandao wake wa YouTube.

Katika wimbo huo kuna baadhi ya mistari na melodi inafanana na wimbo wa Omary uitwao ‘Nifagilieni’, huku tofauti ikiwa wimbo wa Zuchu umeimbwa kisasa zaidi (Bongo Fleva).

Mbali na wimbo huo, ngoma nyingine ni ile aliyomshirikisha Diamond ‘Wale Wale’ ambao umeendelea kufanya vizuri YouTube. Msanii huyo aliingia tena katika hazina ya nyimbo za marehemu kaka yake na kuchukua mistari.

Katika wimbo huo, Zuchu ametumia mstari unaosema, “Chote ni choyo usijali wao kitawaumiza,” mstari ambao uliwahi kusikika kwenye wimbo wa Omary uitwao ‘Imetulia Hiyo’.

Hata hivyo, mbali na msanii huyo kuruka na mistari ya kaka yake, lakini pia amewahi kutumia jina la wimbo ‘Hakuna Kulala’ ambalo jina hilo hilo limewahi kutumika katika wimbo maarufu za Omary Kopa.

Aidha baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimpongeza msanii huyo kuendelea kuenzi kile kilichoachwa na kaka yake. Huku baadhi wakimnanga wakidai kuwa ameishiwa mistari ndio maana nyimbo zake nyingi kwa sasa zimekuwa zikitegemea kazi za marehemu kaka yake.

Kwa namna hiyo, licha ya Omary Kopa kuondoka duniani akiwa bado kijana, kazi zake zinaendelea kusikika na kuishi kupitia sauti ya mdogo wake Zuchu, ambaye anaonekana kuuenzi urithi wa kaka yake kwa namna ya kipekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *