KONA YA MALOTO: Trump anaiua kiuhakika sera ya nje ya MarekaniKONA YA MALOTO: Trump anaiua kiuhakika sera ya nje ya Marekani

Januari 9, 2018, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Marekani, Brendan Boyle, aliwasilisha kwa mara ya kwanza kwenye Mkutano wa 115 wa Congress, mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Kampeni za Uchaguzi ya mwaka 1971, kutaka wagombea wawe wanapimwa akili na majibu yatangazwe hadharani kabla ya uchaguzi. Muswada huo wa sheria ulipewa namba HR 4742.

Mapendekezo hayo ya Sheria ya Kampeni za Uchaguzi hufahamika zaidi kama “Stable Genius Act”. Na inafahamika kuwa stable genius ni namna ambavyo Rais Donald Trump alikuwa akijiita, akimaanisha kwamba yeye ni mwenye akili nyingi zisizoyumbishwa.

Stable Genius Act, asili yake ni wasiwasi kuwa Trump hayupo timamu, hivyo nchi haikupaswa kurudia makosa kuchagua mtu pasipo kujua hali ya afya yake ya akili. Mantiki hasa ni kuwa jinsi Trump hujiamini ana akili nyingi ni hali ya kujiamini kupitiliza (over confidence). Na hiyo ndiyo hasa changamoto ya akili.

Ni kwa sababu hiyo, maneno “stable genius” yamekuwa yakigeuzwa kutoka tafsiri yake kuwa ni mtu mwenye akili zisizoyumbishwa hadi kumaanishwa “mtu mwenye dosari kiakili”. Ndiyo sababu mapendekezo ya Sheria ya Kampeni za Uchaguzi kuitwa Stable Genius Act.

Mapendekezo hayo ya sheria yaliwasilishwa kwa mara ya pili Julai 12, 2019 kwenye Mkutano wa 116 wa Congress, muswada namba HR 3736. Hata hivyo, baada ya uwasilishwaji wa mara ya pili, hakuna hatua yoyote ambayo ilichukuliwa. Kisha, Trump aligombea urais mwaka 2020 na 2024, bila sharti la kupimwa akili. Halafu, alishinda urais kwa mara ya pili Uchaguzi wa Rais 2024, balaa la dunia likawasili hapo.

Februari 28, 2025, Trump alimwalika Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, katika mkutano uliofanyika Ikulu ya Marekani, White House, ndani ya Ofisi ya Rais, The Oval. Mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, uligeuka kituko cha dunia, baada ya Trump na Vance kuchagua kumsuta Zelenskyy, badala ya kuzungumza kistaarabu kuhusu namna bora ya kumaliza vita ya Ukraine na Urusi.

Kipindi ambacho sera ya Marekani ya nje ikiwa kujipambanua kama mlinzi wa demokrasia, usawa na utawala wa sheria duniani, Trump aliivua nguo nchi hiyo kwa kuivamia Venezuela, akamng’oa madarakani aliyekuwa Rais, Nicolas Maduro. Trump hakusubiri, akatangaza waziwazi mpango wa Marekani kunufaika na mafuta ya Venezuela.

Sakata la Greenland limepoa kiasi, hasa baada ya Trump kwa kushirikiana na Israel kuivamia Iran, ambayo iliamua kujibu mashambulizi na kuishangaza dunia kuhusu nguvu na maarifa yake ya kijeshi na kivita. Trump alikuwa anataka kukitwaa kisiwa cha Greenland, akidai ni kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, inafahamika kwamba Greenland ina utarjiri mkubwa wa madini.

Greenland ina ukubwa wa kilometa za mraba milioni 2.2. Inaweza kulingana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) au Saudi Arabia. Uchumi wa Greenland, kwa miaka yote, unategemea shughuli za uvuvi, pamoja na ruzuku kutoka Denmark.

Ipo nuru ing’aayo Greenland miaka ya karibuni. Ni nuru ya rasilimali. Imegundulika kuwa Greenland ina utajiri mkubwa wa madini adimu, vilevile uranium na chuma. Ni hiki ndicho kinamfanya Trump aimezee mate Greenland.

Wakati ukiiwazia kesho ya Greenland, usisahau nadharia ya Trump ya kuifanya Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani. Kwa sasa, na kwa karne zaidi ya mbili, Marekani inatambulika kuwa ni nchi ya muungano wa majimbo 50. Trump anataka kuiongeza Canada.

Kuhusu Iran, ipo wazi ni uvamizi ambao umeshindwa. Trump ameiingiza dunia kwenye janga kubwa la kupanda kwa gharama za maisha. Majibu ya Iran ya kuufunga mlango bahari wa Hormuz, yamechochea kupanda kwa gharama za mafuta ulimwenguni.

Trump alifanya uamuzi wa kuivamia Iran kijeshi kwa upacha mkubwa ba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Hata hivyo, misimamo ya Trump yenye kuyumba kila mara, imesababisha msuguano baridi baina ya Tel Aviv (Israel) na Washington DC (Marekani), kuhusu namna ya kuendelea na vita au kusitisha.

Ndani ya siku moja, Trump anaweza kutoa kauli hata tano zinazosigana. Tabia hiyo imekuwa ikishusha hadhi ya Ofisi ya Rais wa Marekani, na inapunguza kuaminika kwa nchi hiyo. Kwa miaka yote, Marekani imekuwa mtetezi wa Taiwan kujitenga na China. Trump alipokuwa ziarani China Mei 13 – 15, 2026, aliionya Taiwan kujitangaza kuwa dola huru.

Kauli hiyo ya Trump ilikuwa sawa na kofi la usoni kwa Taiwan kutoka Marekani. Hata hivyo, upo wito wa kudharau matamshi ya Trump kwa sababu hutokea kuzungumza kauli nyingi zinazopishana ndani ya muda mfupi. Mwandishi wa Canada, mwenye makazi yake Taipei, Taiwan, J Michael Cole, aliitaka Serikali ya Taiwan kutozingatia kauli za Trump.

“Tunatakiwa kuweka akilini kuwa Trump ana kawaida ya kusema vitu vingi, wakati mwingine anajichanganya yeye mwenyewe ndani ya saa 24, inategemea nini amesikia kwa wakati huo, na amezungumza na nani,” alisema Cole, katika ushauri wake wenye maana ya kumpuuza Trump.

Wakati huohuo, taarifa zilizokusanywa na Akili Unde (AI), zinaonesha kuwa Trump ameshatoa taarifa zaidi ya 30,000, ambazo zilithibitika kuwa hazikuwa kweli. Hii inaongeza uzani kwenye hoja kuwa Trump si wa kumzingatia.

Jumamne, Mei 19, 2026 (jana), gazeti la The New York Times, lilichapisha ripoti yenye kuonesha kuwa Wamarekani asilimia 64, wanapinga nchi yao kuingia vitani dhidi ya Iran. Ongeza maandamano ya kumpinga Trump yenye jina “No Kings”, yenye maana ya kutotaka wafalme kwenye nchi hiyo. Dhahiri, Trump anapitia upinzani mkali nchini mwake kuelekea uchaguzi wa nusu muhula unaotarajiwa kufanyika Jumanne, Novemba 3, 2026.

Hofu ya Trump ni kuwa endapo chama chake kitapoteza viti vingi kwenye Congress, atang’olewa madarakani. Hata hivyo, ukweli ni kuwa urais wa Trump umekuwa na matokeo makubwa ya kusigina sera ya nje ya Marekani. Nguvu ya ushawishi (soft power), ya Marekani, imepwaya mno kipindi cha pili cha urais wa Trump.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *