Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz amefanikiwa kuweka rekodi nyingi katika muziki Tanzania na Afrika kwa ujumla, kitu ambacho kimemjengea heshima kubwa kwa mashabiki.
Hata hivyo, kadiri muda unavyozidi kwenda Diamond amepoteza pia rekodi zake nyingi, lakini kwa leo tunakuletea 10 ambazo bado anazishikilia katika tasnia hiyo.
1. Ikiwa ni miaka 17 tangu ametoka rasmi kimuziki, Diamond ndiye mwanamuziki aliyeshinda mara nyingi zaidi Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kwa muda wote akiweka kabatini tuzo zaidi ya 22. Mara ya mwisho tuzo hizo kufanyika hapo Oktoba 2024, Diamond alishinda vipengele vinne Mtumbuizaji Bora, Video Bora (Achii), Wimbo Bora wa Dansi (Achii), na Msanii Bora wa Kiume.
2. Bado anashikilia rekodi ya kushinda saba za TMA kwa usiku mmoja akifanya hivyo msimu wa 2014, huku 20 Percent, Alikiba na Zuchu wakiondoka na tuzo tano kila mmoja kwa misimu ya 2021, 2015 na 2021.
3. Ndiye mwanamuziki mwenye ushawishi zaidi katika mitandao ya kijamii Afrika Mashariki na Kati, akiwa ni namba moja kwa kuwa na wafuasi wengi katika mitandao ya Instagram, Facebook, X, TikTok na YouTube.
4. Diamond ndiye mwanamuziki wa Afrika Mashariki aliyeshinda mara nyingi zaidi katika tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) ambapo ameshinda tuzo nane kati ya mwaka 2015 hadi 2022. Tuzo za AEAUSA zilianza kutolewa Oktoba 2015 huko New Jersey, Marekani zikiwa na vipengele 30 kuhusu muziki na mambo mengine kwa wasanii na watu wengine wa Afrika katika tasnia ya burudani.
5. Bado ndiye mwanamuziki mwenye wafuatiliaji (subscribers) wengi katika mtandao wa YouTube barani Afrika akiwa nao milioni 11.4. Mnamo Juni 2025, alikabidhiwa tuzo (Diamond Creator Award) ambayo hutolewa kwa kufikisha wafuatiliaji milioni 10.
Hivyo ndiye mwanamuziki wa kwanza kupokea tuzo hiyo kutokea YouTube ikiwa ni ya tatu baada ya hapo awali kupokea Silver Creator Award (kwa wafuatiliaji 100,000) na Gold Creator Award (1,000,000).
6. Diamond ni mwanamuziki wa kwanza Afrika Mashariki kuingiza wimbo (Komasava) katika chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs, na hadi sasa hakuna msanii mwingine aliyeweza kuifikia rekodi hiyo.
7. Diamond ndiye msanii pekee kutokea Afrika Mashariki mwenye video nyingi ambazo zimetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 YouTube.
Anazo video sita zenye namba hizo ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Nana (2015), Jeje (2020), na African Beauty (2018).
8. Baada ya Diamond, wote wanaomfuatia wana video moja moja, video ya Harmonize iliyofanya hivyo ni Kwangwaru (2018), Zuchu ni Sukari (2021), Jux ni Enjoy (2023) na Rayvanny ni Number One (2020).
9. Diamond anaongoza Afrika kwa kushinda tuzo nyingi za MTV Europe Music Awards (EMAs) ambapo mwaka 2015 alishinda mbili ikiwa ni mara ya kwanza msanii wa Afrika kufanya hivyo, na 2023 akashinda moja.
10. Mshindi wa Grammy mara mbili kutokea Afrika Kusini, Tyla naye ameshinda tatu ila yeye alichukua zote kwa msimu mmoja huku akiweka rekodi ya kuwa mwafrika wa kwanza kushinda kipengele cha Best R&B ndani ya MTV EMAs.
