UCHAMBUZI WA MJEMA: Kwa aina hii ya vyama, bora tuwe na mgombea binafsiUCHAMBUZI WA MJEMA: Kwa aina hii ya vyama, bora tuwe na mgombea binafsi

Ukisoma takwimu za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tanzania ina vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu 19, lakini kwa mienendo ya baadhi ya vile vya upinzani, natamani tuwe na Katiba mpya inayoruhusu mgombea binafsi 2030.

Licha ya uwepo wa utitiri wa vyama hivyo, vinavyoonekana kutekeleza majukumu ya kisiasa ya ukweli havizidi vinne na vingine kutajwa kuwa ni “project” ya chama tawala CCM na hii imefanya wananchi walio wengi, kupoteza imani navyo.

Kwa tathmini yangu mimi kama utaniuliza, nitakuambia chama cha upinzani kinachotekeleza majukumu yake ya kisiasa kwa asilimia 100 ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), licha ya misukosuko kinachopitia.

Vyama vingine ni ACT Wazalendo, NCCR Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) lakini vyama vingine havisikiki, havionekani katika shida za Watanzania na baadhi husimama upande tofauti na wananchi na hujitokeza tu nyakati za uchaguzi.

Wala hatusikii ni lini walifanya mikutano na vikao kwa mujibu wa Katiba zao, bali vinaibuka tu nyakati za uchaguzi au wakati wa kutoa matamko ambayo wakati mwingine wananchi tunashika vichwa tunajiuliza, hivi hawaoni matatizo yetu?

Leo kuna baadhi ya viongozi wa vyama hivyo ninavyovizungumzia ukiwauliza ni lini mara ya mwisho walifanya mkutano wa hadhara na wapi na mwitikio wa wananchi ulikuwaje hawawezi kukupa jibu, vimepoteza uhalali wa kisiasa. Huo ndio ukweli.

Bahati mbaya sana, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo vya siasa vya upinzani wanadhani Watanzania wale wa wakati Tanzania inapata uhuru ndio hawa hawa wa kizazi cha Gen Z, wanajidanganya, Watanzania hawa ni waelewa kuliko.

Katika mazingira hayo, ni mwananchi mpenda demokrasia yupi anaviona vyama hivyo ni kimbilio kwao zaidi ya kujenga hisia kuwa baadhi ya viongozi wao wapo hapo kwa ajili ya matumbo yao, kusaliti watanzania na kulamba asali.

Nchi iko kwenye majaribu makubwa hivi sasa, vyama hivi viko wapi kuusema ukweli wa kabla, Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata? Badala yake tunasikia tu Chadema, ACT-Wazalendo, CUF na NCCR Mageuzi.

Ni kweli Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Tanzania ya 1977 inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini swali tuna vyama vingapi makini vya upinzani?

Katiba yetu hiyo ambayo kwa hakika imepitwa na wakati na sheria zingine zinazosimamia chaguzi zetu, inasema ili kugombea nafasi ya mwenyekiti wa kijiji au kitongoji, udiwani, ubunge na urais ni lazima udhaminiwe na chama cha siasa.

Sasa unajiuliza, kwa wale wasio na chama wanapataje haki ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa? Au wale ambao hatukubaliani na sera za vyama hivyo 19 tunapataje haki yetu ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa?

Kwa sababu ni ukweli haiwezekani Watanzania wote wakawa ni CCM kwamba wanagombea ndani ya chama hicho chenye uongozi imara, mifumo imara ya kiuongozi hadi ngazi ya shina, wapo wanaotamani vyama vingine vya siasa.

Sasa wale wanaotaka kugombea nje ya CCM na ukizingatia aina ya baadhi ya vyama vya upinzani tulivyonavyo ambavyo hata mikutano ya hadhara ya kuimarisha uhai wa chama ni mtihani, ndio wananchi wataviunga mkono?

Ni kweli na wala hili hatubishani kwamba Chadema ndicho chama kikuu cha upinzani nchini, lakini kinavyopitishwa kwenye tanuru la moto hadi hakikushiriki uchaguzi mkuu 2025, wananchi wanaipataje haki yao ya kikatiba?

Majawabu ya mkwamo huu ni uwapo wa mgombea binafsi au mgombea huru.

Sielewi kabisa kwanini CCM na Serikali yake haitaki kusikia suala la mgombea binafsi au mgombea huru kwa sababu akina Mchungaji Christopher Mtikila na wengine walishashinda kesi juu ya suala hili, serikali ya CCM inalikatia rufaa.

Mwaka 2013 baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, ilikuja na Ibara ya 75(g) ya Rasimu ya Katiba na kuingiza takwa la Kikatiba la uwepo wa mgombea huru katika chaguzi zetu.

Katiba Inayopendekezwa ambayo safari yake iliishia njiani baada ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliotokana na CCM, ambao walikuwa wengi, kutanguliza maslahi yao ya kisiasa na kuondoa mambo mengi ya wananchi.

Sasa kwa mazingira ya kisiasa ya nchi yetu kwa sasa na kwa yale niliyoyaelezea hapo awali, suala la mgombea huru haliepukiki hivyo tutakaporudisha mchakato wa Katiba mpya, suala hilo ni muhimu sana kama mgonjwa na uji.

Haiwezekani tuwe na Katiba inayomlazimisha kila mtanzania anayetaka kugombea nafasi ya kisiasa katika vyombo vya Dola awe ni mwanachama wa chama cha siasa na adhaminiwe na chama cha siasa, huku ni kukiuka haki zao za Kikatiba.

Majirani zetu Kenya na Uganda wao Katiba, Sheria na Kanuni zao zinaruhusu uwepo wa wagombea binafsi na mathalan, katika uchaguzi mkuu wa Kenya 2021, wagombea binafsi au huru 74 walishinda viti vya ubunge kati ya viti 529.

Katika uchaguzi mkuu wa Kenya 2022, wagombea 12 huru au binafsi walishinda viti vya ubunge, lakini kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), kulikuwa na jumla ya wagombea binafsi 3752 katika nafasi mbalimbali.

Wanazuoni Denis Kamugisha na Idda Swai wameelezea kwa kirefu umuhimu wa mgombea huru kupitia andiko lao la ‘Inclusion of Independent Candidates in the Electoral System in Tanzania: A Monster to Men and Women Contenders?’

Wanasema kujumuisha wagombea binafsi katika mfumo wa uchaguzi wa Tanzania kumetazamwa kwa muda mrefu kama jinamizi (monster), hali inayoashiria mifumo migumu inayokandamiza sauti za kidemokrasia hapa Tanzania.

Mifumo ya kisheria ya uchaguzi (election legal framework) inadhoofisha uchaguzi jumuishi na shirikishi mara kwa mara kwa wagombea huru kuwekewa vikwazo vya kisheria, na ndio maana nasema tudai mgombea huru kwa nguvu zote.

Hatuwezi kuwa na taifa ambalo Katiba yake inalazimisha kila mwananchi anayetaka kugombea nafasi za kisiasa katika vyombo vya Dola, awe ni mwanachama wa chama cha siasa hata kama hakubaliani na Itikadi yake.

Ukiacha hoja hiyo, lakini tujiulize ni vyama gani vya siasa ambavyo mwananchi ambaye ni huru na asiye na imani katika itikadi za vyama, analazimishwa kujiunga kuwa mwanachama, ukiondoa CCM, Chadema na vile vingine nilivyovitaja.

Sielewi hofu ambayo CCM na Serikali yake inayo inasababishwa na nini.

Tuliingize kwenye Katiba na kwa kuwa Tume ya Jaji Chande imependekeza Katiba mpya iwe tayari ifikapo 2028 ili iweze kutumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2029 na uchaguzi mkuu 2030, tuanze sasa na si kesho juu ya suala hili.

Kuzuia Katiba mpya itakayozaa Tume Huru ya Uchaguzi, Bunge Huru, Mahakama Huru na Taasisi Imara ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mikono na tusisubiri wananchi wakadai mabadiliko ya Katiba kwa nguvu ya umma, ndiko tunaeekea.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania – 0656600900.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *