
Rais wa Kenya, William Ruto anapitia nyakati ngumu kama kiongozi wa taifa hilo kutokana na mfululizo wa matukio na mwenendo wa siasa zinazoendelea nchini humo ukiwa umesalia takribani mwaka mmoja kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Kenya inatarajia kwenda kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2027 ambapo Ruto anatarajia kuwania muhula wa pili ili kukamilisha mihula miwili ya miaka mitano mitano, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kenya ya mwaka 2010.
Muhula wake wa kwanza ambao sasa umefikisha karibu miaka minne, umetawaliwa na minyukano mikali kati yake na wananchi, pamoja na wanasiasa wa upinzani ambao wana ushawishi mkubwa nchini humo.
Mara kadhaa wananchi wake waliitisha maandamano kulalamikia kupaa kwa gharama za maisha huku wakiisukumia lawama Serikali yake kwamba imeshindwa kuchukua hatua kupunguza makali ya maisha.
Wakati muda ukiendelea kwenda mbio kuelekea uchaguzi mkuu, Rais Ruto amekuwa akikosolewa kwa kutotekeleza ahadi nyingi alizozitoa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, jambo linalomweka mbali na wananchi wake.
Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa akipigia upatu baadhi ya mambo ambayo ameyafanya ikiwamo ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, jambo linalokosolewa na wapinzani kwamba siyo mahitaji ya msingi ya wananchi.
Makala haya yanabainisha baadhi ya mambo yanayoendelea kumweka katika nafasi ngumu Ruto kwenye siasa za Kenya huku naye akipambana kujinasua ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Gharama za maisha
Ikiwa imepita miaka michache tangu maandamano makubwa ya kupinga muswada wa fedha uliopendekeza kuongeza kodi, mgomo wa daladala ulifanyika juzi nchini humo kupinga kupaa kwa bei ya mafuta kulikochochewa na mzozo unaoendelea Mashariki ya kati.
Katika mgomo huo, baadhi ya waendesha daladala hizo pamoja na vikundi vya waandamanaji walifunga baadhi ya barabara muhimu kwa kuweka mawe na kuchoma matairi huku shughuli zikisimama katika jiji la Nairobi.
Takribani watu wanne wamepoteza maisha kwenye mgomo na maandamano hayo huku wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen.
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini Kenya ilipandisha bei za rejareja za mafuta kwa hadi asilimia 23.5 wiki iliyopita, baada ya kuongeza kwa asilimia 24.2 mwezi uliopita, kufuatia vita vya Mashariki ya Kati vinavyokwamisha usambazaji wa mafuta na gesi duniani.
Mgomo huo umetokea wakati Rais Ruto akiwa Azerbaijan ambako amekwenda kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Miji Duniani (WUF13), jambo ambalo wakosoaji wake wanasema aliondoka bila kutoa neno la matumaini kwa wananchi kufuatia tetesi za kutokea kwa mgomo huo.
Kupaa kwa bei ya mafuta nchini humo, kunaendelea kumweka kwenye wakati mgumu kiongozi huyo kwani wananchi wake hawamwelewi licha ya kwamba changamoto hiyo siyo ya Kenya pekee, bali mataifa mengi ya Afrika.
Licha ya serikali kutangaza kushusha bei ya mafuta, mgomo huo uliingia siku ya pili jana huku wananchi wakipata changamoto ya usafiri kwenda kwenye shughuli zao za kila siku, wengine wakiamua kutembea.
Kutengana na Gachagua
Kumteua Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, ilikuwa kete muhimu ya ushindi kwa Ruto kutokana na Gachagua kutoka eneo la Mlima Kenya lenye idadi kubwa ya wapigakura nchini humo.
Hata hivyo, wawili hao waliweza kufanya kazi pamoja kwa kipindi kifupi cha miaka miwili ya kwanza ambapo Gachagua akiwa Naibu wa Rais, alipigiwa kura na Bunge ya kukosa imani naye, hivyo kuondolewa katika nafasi hiyo.
Maana yake ni kwamba, Ruto kugombana na mshirika wake huyo amejiweka mtegoni katika eneo la Mlima Kenya kwa sababu Gachagua ana wafuasi wake wengi ambao awali walikuwa wa Ruto pia, lakini sasa siyo wake.
Hivyo, anahitaji kuanza upya kujenga ushawishi wake kwa wananchi wa eneo hilo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye uchaguzi ujao, ikiwemo kuvuna kura nyingi katika eneo hilo muhimu katika siasa za Kenya.
Mbali na hilo, Gachagua ameanzisha chama chake cha DCP na amekuwa akifanya mikutano mbalimbali akihamasisha wananchi kumng’oa Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao ili awe Rais wa muhula mmoja, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa viongozi waliotangulia nchini humo.
Wakati anapambana kujiimarisha na chama chake, kwa namna fulani anapunguza nguvu ya Ruto, mshirika wake wa zamani, na huenda wawili hao wakatengeneza mchuano mkali kwenye uchaguzi ujao.
Tofauti zake na Kenyatta
Rais wa zamani, Uhuru Kenyatta ndiye mstaafu pekee aliyebaki katika ngazi ya Rais nchini humo, hivyo ana mengi ya kushauri au kuelekeza hasa kipindi cha nyakati ngumu kama maandamano au migomo inayotokea.
Hata hivyo, licha ya kuwa katika uhusiano hafifu, Kenyatta anaongoza chama cha Jubilee ambacho nacho kina malengo ya kutoa mgombea urais kwenye uchaguzi ujao na kuhakikisha anashinda uchaguzi huo.
Ruto na chama chake cha UDA, wanahitaji kupata washirika wengi zaidi ili kujihakikishia ushindi kwenye uchaguzi ujao, hata hivyo siyo Jubilee kutokana na uhusiano wake na mtangulizi wake uliolegalega.
Hakika, uhusiano mzuri na mtangulizi wake ungempa unafuu siyo tu katika kuongoza nchi, bali pia kuunganisha vyama vyao ili kupata nguvu zaidi ya kuwashinda wapinzani ambao nao wana nguvu kubwa isiyo ya kubeza.
Uzoefu na busara za Kenyatta zimeweza kumsaidia kufanya vizuri kwenye uamuzi anaoufanya ili kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuifanya Kenya kuwa nchi tulivu, inayoheshimika na wananchi wake wanajivunia.
Mgogoro ndani ya ODM
Chama cha upinzani cha ODM kimeingia kwenye mzozo baina ya viongozi wake baada ya kufariki kwa kiongozi wake, Raila Odinga ambaye alitengeneza uhusiano na Ruto kiasi cha chama hicho kujumuishwa serikalini.
Pande mbili ndani ya chama hicho zinakinzana ikiwamo upande unaoongozwa na Oburu Odinga, kaka yake Raila, unaotaka ODM kiendelee kumuunga mkono Ruto na upande mwingine unaoongozwa na Katibu Mkuu, Edwin Sifuna, unataka ODM kibaki kama chama cha upinzani kumkabili Ruto kwenye uchaguzi ujao.
Kundi la vijana wengi ndani ya chama hicho wako nyuma ya Sifuna wakitaka ODM kiendelee kuwa chama cha upinzani chenye nguvu kama kilivyokuwa wakati wa uongozi wa Raila katika nyakati zote tangu kuanzishwa kwake.
Mgogoro huo wa ndani ya ODM una athari kwa Ruto kwani anakosa washirika ambao angeshirikiana kumwezesha kupata kura nyingi kwenye uchaguzi ujao, ukizingatia kwamba chama hicho kina wafuasi wengi hasa katika eneo la Nyanza.
Ruto anawahitaji ODM wakiwa na umoja ili kubeba nguvu yao kwenye uchaguzi kama washirika wanaoweza kumwongezea kura Agosti 2027 na kumfanya aendelee na muhula wake wa pili wa miaka mitano kama Rais wa Kenya.
Imani ya wananchi yapungua
Wakati anaingia madarakani, Ruto aliahidi kuwainua Wakenya wenye hali duni kimaisha, akiwaita “hustlers”. Hata hivyo, tangu ameingia madarakani, hajafanikiwa kukata kiu ya Wakenya kwa viwango vya kuridhisha.
Mbali na kuwawezesha kimaisha, Ruto analaumiwa kwa kuongeza kodi mara dufu wakati gharama za maisha zikiwa juu kuliko wakati wa nyuma. Pia, bili za umeme, chakula na nyumba vimepanda nchini humo na kufanya maisha ya wananchi kuwa magumu.
Vilevile, vijana wengi nchini humo wanalalamika kwamba hawana ajira huku wakimlaumu kiongozi huyo kwamba hajatimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba wanapata ajira ili kujikimu kimaisha kama watu wengine.
Wakosoaji wake wamekuwa wakidai kwamba amekuwa mtu wa kutoa ahadi lakini hatekelezi, kuanzia kwenye ujenzi wa barabara, viwanja vya mpira na kuinua maisha ya walala hoi wanaohangaika kupata mkate wao wa kila siku.
Mchambuzi ammulika
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo anasema Ruto ni mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kisiasa ndani ya Kenya, lakini tofauti na kipindi cha mwanzo wa utawala wake, sasa anakabiliwa na mazingira magumu zaidi kisiasa na kijamii.
Anasema ni vigumu kumdharau kisiasa kutokana na uzoefu wake, mtandao wake wa kisiasa na uwezo wake wa kujenga miungano, lakini pia ni wazi kuwa kiwango chake cha umaarufu kimepungua katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Kwanza, anasema lazima ikubalike kuwa Ruto ni mmoja wa wanasiasa wajanja zaidi katika historia ya siasa za Kenya za karibuni. Hata hivyo, changamoto kubwa inayomkabili sasa ni hali ya uchumi na matarajio ya wananchi.
“Wakenya wengi leo wanapima utawala wake kwa gharama ya maisha, kodi, ajira na hali ya uchumi kwa ujumla. Kila serikali inapokaa madarakani kwa muda, siasa za matumaini hupungua na nafasi yake kuchukuliwa na siasa za tathmini ya utendaji. Hapo ndipo Ruto anakutana na ukosoaji mkubwa Zaidi,” anasema.
Pia, Shoo anasema maandamano ya vijana yaliyoshuhudiwa katika vipindi vya hivi karibuni yanaonesha kuwa kuna sehemu ya kizazi kipya ambayo imeanza kuonyesha kutoridhishwa na mfumo mzima wa kisiasa, si kwa Ruto pekee bali kwa tabaka lote la viongozi wa kisiasa nchini Kenya.
Anasema hiyo ni ishara muhimu kisiasa kwa sababu Kenya ina idadi kubwa ya vijana wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na mjadala wa kitaifa.
“Kusema kwamba Ruto hana ushawishi itakuwa ni tafsiri isiyo sahihi kisiasa. Bado ana nguvu ndani ya taasisi za serikali, ana uwezo mkubwa wa kisiasa katika maeneo ya Rift Valley na sehemu nyingine muhimu, na bado ana uelewa mkubwa wa namna ya kuendesha siasa za muungano nchini Kenya. Wanasiasa wengi wa Kenya bado wanaonekana kujipanga kisiasa kwa kuzingatia nafasi yake ndani ya dola,” anasema mwanazuoni huyo.
Hata hivyo, anasisitiza kwamba Ruto bado ana ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya, lakini sasa anapambana zaidi kulinda uhalali wa kisiasa kuliko kujenga matumaini mapya. Na katika siasa za Afrika Mashariki, anasema hiyo ndiyo hatua ngumu zaidi kwa kiongozi yeyote aliyeko madarakani.”
