
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, amesema nchi ya Msumbiji imefanikiwa kupata fedha kwa ajili ya vikosi vya Kigali vilivyoko nchini humo kuendelea na operesheni za kijeshi kwa mji wa Cabo Delgado, ambako wanajihadi wa kiislamu wanatatiza usalama.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kigali iliwatuma wanajeshi wake kaskazini mwa Msumbiji mwaka wa 2021 kwa ombi la Msumbiji kusaidia kurejesha utulivu katika baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yakikaliwa na makundi ya magaidi wanaohusishwa na Islamic State.
Ujumbe wa wanajeshi wa Rwanda kwa sehemu ulikuwa ukifadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Kigali ikisema EU ilianza kusitasita kutoa ufadhili huo.
Kupitia ukurasa wake wa X, Nduhungirehe amesema Msumbiji kwa sasa imefanikiwa kupata ufadhili wake yenyewe ambapo wanajeshi wa Rwanda wataendelea kusalia nchini humo.
Licha ya kuthibitisha hatua hiyo, hakuweka wazi ni ufadhili wa kiasi gani ambao Msumbiji imepata kwa ajili ya oparesheni za kijeshi za Rwanda na itafanyika kwa muda upi.
Rwanda mwezi Machi ilikuwa imeonya kuwa ingewaondoa wanajeshi wake nchini Msumbiji kutokana na uhaba wa ufadili baada ya EU kutangaza kuwa ilikuwa inapanga kujiondoa kwenye mpango huo.
