
Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, Amani Golugwa amesema David Jumbe, msaidizi wa mwenyekiti wa Chama hicho, Tundu Lissu amepatikana akiwa na pingu mkononi.
Amesema taarifa hizo amezipata hivi punde kutoka kwa mke wa Jumbe ambaye amethibitisha mumewe kurejea nyumbani akiwa na pingu mikononi.
Golugwa amesema Jeshi la Polisi waliofika makao makuu ya Chadema leo Alhamisi, Mei 21, 2026 saa tatu asubuhi walijitambulisha wanatoka kituo cha Polisi Oysterbay na wanamtafuta Jumbe ambaye walidai alitoweka na pingu.
Kwa mujibu wa Golugwa, askari hao wamedai Jumbe alijificha ndani ya Ofisi za Chadema hivyo wanamtaka wamfungulie pingu.
“Tunawaambia Polisi Jumbe yupo nyumbani kwake waende kumfungulia pingu,” amesema Golugwa.
Awali, taarifa zilizosambaa mitandaoni zilieleza David anadaiwa kuchukuliwa nyumbani kwake Mabwepande, Bunju jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Alhamisi. Taarifa hiyo inayodaiwa kuwa ni maelezo ya mke wa Jumbe ilisema:
“Jumbe alikuwa anarudi nyumbani na alipofika getini alifuatwa na watu hao, wakamkamata na kumwingiza kwenye gari aina ya Land Cruiser kisha kuondoka kwa mwendo mkali.
“Jumbe alipiga kelele na kujaribu kujitetea lakini watu hao wakamzidi nguvu. Majirani walipofika walijaribu kuikimbiza gari hiyo bila mafanikio,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika purukushani hizo, Jumbe anadaiwa kudondosha kiatu alichokuwa amevaa kabla ya kuchukuliwa na watu hao ambao hawakujitambulisha kwa familia.
Mwananchi inaendelea kumsaka Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kwa ufafanuzi kuhusu tukio la kuhojiwa kwa Golugwa na madai ya kutoweka kwa David Jumbe.
