Tanzania yasisitiza ushirikiano wa kikanda kupambana na ujangiliTanzania yasisitiza ushirikiano wa kikanda kupambana na ujangili

Nairobi. Serikali ya Tanzania, imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na biashara haramu ya mazao ya misitu inayovuka mipaka ya nchi.

Hayo yameelezwa jijini Nairobi nchini Kenya, na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la 14 la Uongozi wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka.

Amesema mapambano dhidi ya ujangili hayawezi kushinda bila ushirikiano wa pamoja wa mataifa ya Afrika.

Dk Kijaji ambaye pia ni Rais wa baraza hilo, amesema mitandao ya uhalifu wa wanyamapori imekuwa ya kimataifa zaidi, hivyo inahitaji majibu ya pamoja yanayovuka mipaka ya kitaifa.

Amebainisha kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha mikakati ya uhifadhi, ikiwemo uhifadhi shirikishi unaowashirikisha wananchi wanaoishi karibu na hifadhi.

Ameongeza kuwa mafanikio ya uhifadhi hayategemei matamko pekee bali utekelezaji wa vitendo, uwekezaji, ubunifu na mifumo imara ya ufuatiliaji na usimamizi wa rasilimali.

Aidha, amesisitiza kuwa wanyamapori na misitu si mali ya nchi moja pekee bali ni urithi wa dunia unaopaswa kulindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kikao hicho kimewakutanisha pia nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka zikiwemo Kenya, Tanzania, Congo Brazzaville, Zambia na Liberia.

Majadiliano hayo yametokana na maazimio ya kikao kilichopita kilichofanyika Mei 2025 jijini Arusha, Tanzania.

Katika kikao hicho, Dk Kijaji pia amezindua Mpango Mkakati wa Sekretarieti ya Mkataba huo kwa kipindi cha 2025/30, unaolenga kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori na uharibifu wa misitu katika ukanda wa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *