
Dar es Salaam. Siku moja baada ya David Djumbe, msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kunusurika kutekwa akielekea nyumbani kwake, wadau wa siasa na haki za binadamu wamesema kinachohitajika ni utashi wa kisiasa ili kumaliza matukio ya aina hiyo.
Mbali na hilo, wadau hao wameshauri Rais Samia Suluhu Hassan aunde tume ya kuchunguza wahusika wa matukio hayo ili watakaobainika wawajibishwe kisheria.
Maoni hayo ya wadau yanakuja siku moja baada ya kusambaa taarifa za Djumbe kutekwa akielekea nyumbani kwake Bunju akiwa na rafiki yake, Allan Macha wakiwa kwenye gari, kabla ya kufanikiwa kujiokoa akiwa hoi na pingu mkononi.
Djumbe ambaye Mei 21, 2026 aliripoti Kituo cha Polisi Osterbay ili kuondolewa pingu alizofungwa na watekaji, ameeleza namna alivyowatoroka watekaji.
Kwa mujibu wa Djumbe, baada ya watekaji kumchukua na kuanza kukimbia naye, rafiki yake aliomba msaada kwa majirani, ndipo maderava pikipiki walikimbiza gari lililombeba kwa lengo la kulizuia.
Baada ya gari lililombeba kufika Mbweni, walishuka ili kuwadhibiti bodaboda na hapo Djumbe aliyewekwa kwenye buti la gari la watekaji aina ya Toyota Probox alipata fursa ya kuchoropoka na kurukia porini na hapo ndipo akanusurika mikononi mwa watekaji hao.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupitia taarifa iliyoitoa kwa umma Mei 21, 2026, uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kuwabaini wahusika ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Utash wa kisiasa
Akitoa suluhu ya matukio ya utekaji nchini, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Paul Loisulie amesema ili matukio hayo yakomeshwe Serikali inapaswa kuyadhibiti.
“Serikali ifike sehemu isiwe inasikiliza malalamiko tu, sasa ichukue hatua, bila kuchukuliwa hatua matukio haya hayataisha. Changamoto iliyopo ni ya kisiasa na shida hiyo lazima imalizwe kisiasa,” amesema.
Dk Loisulie amesema kama Serikali haitatoa tamko kali na kuchukua hatua dhidi ya matukio ya utekaji hayawezi kukoma.
“Ikifika sehemu wananchi wakakosa matumaini na kuanza kuchukua hatua wenyewe hali itakuwa mbaya. Kwa hiyo Serikali ichukue hatua kabla ya wananchi kuchoka,” amesema.
Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), William Maduhu amesema matukio ya utekaji siyo mapya nchini na kwamba wao wamekuwa wakitoa mbinu za kumaliza tatizo hilo bila mafanikio.
Amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa na kuhusishwa na wivu wa mapenzi, uchawi.
“Sasa ili kumaliza kweli matukio ya utekaji, ni lazima Serikali iwe na utashi wa kisiasa wa kumaliza tatizo hili kwa kuwajibishana kwa sababu kama matukio yanatokea mtu hawajibika, bado yataendelea kutokea,” amesema.
Amesema ni muhimu Rais Samia atoe tamko ili wahusika wote wasakwe na kushughulikiwa kwani tatizo linapozidi kunyamaziwa ndio huendelea kuota mizizi.
Maduhu amesema njia nyingine ya Rais Samia kushughulikia matatizo ya utekaji ni kuunda tume ya kuchunguza na kuwabaini wanaowatuma.
Vivyo hivyo, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Noel Shao amesema matukio ya utekaji yanayotokea sasa ni mwendelezo wa yale yasiyochukuliwa hatua.
“Haya matukio tumeanza kusikia muda mrefu, sasa kama taifa hatuwezi kwenda kwa mwendo huo, tuna vyombo vya ulinzi na usalama lakini matukio ya namna hii yanaendelea kusikika, ni muhimu Rais Samia Suluhu Hassan atoe tamko,” amesema Shao.
Shao amesema ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa kuzingatia sheria wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kukomesha hali hiii.
Amesema matukio hayo yanaleta taswira mbaya kwa taifa na hayapaswi kuonekana ya kawaida kwenye jamii.
