Utafiti wafichua viuatilifu vinavyoweka watoto hatariniUtafiti wafichua viuatilifu vinavyoweka watoto hatarini

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) umeibua hofu kuhusu athari za viuatilifu kwa afya ya watoto na kina mama.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 11 ya wanawake wanaogusana na viuatilifu moja kwa moja wanajifungua watoto njiti huku watoto wengine wakikabiliwa na changamoto ya ujifunzaji darasani.

Matokeo hayo yanaonesha tofauti kubwa ikilinganishwa na wanawake wasiokuwa kwenye shughuli za kilimo au wasiogusana na viuatilifu, ambao uwezekano wao wa kupata watoto wenye changamoto hizo ni asilimia mbili pekee.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika warsha ya siku mbili ya uzinduzi wa mradi wa kikanda wa kupunguza matumizi ya viuatilifu hatarishi (Highly Hazardous Pesticides – HHPs), Mhadhiri na Mtafiti Mwandamizi wa Muhas, Dk Vera Ngowi amesema tafiti mbalimbali zinaonesha viuatilifu vinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya mama na mtoto.

Amesema tofauti na zamani, wanaume ndio waliokuwa wakijihusisha zaidi na upuliziaji wa viuatilifu, sasa wanawake wengi wameingia katika kilimo cha mboga na hushiriki moja kwa moja shughuli za kupulizia, kuvuna na kushika mazao yaliyowekwa kemikali hizo.

“Tunachokiona sasa ni kwamba madhara haya hayaishii kwa mama pekee. Mwanamke anapogusana na viuatilifu baadaye akibeba ujauzito, kemikali hizo zinaathiri pia mtoto aliyepo tumboni,” amesema Dk Ngowi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, watoto wanaozaliwa na kinamama waliogusana na viuatilifu hukumbwa na changamoto mbalimbali za ukuaji wa ubongo na ujifunzaji, hasa wanapoanza elimu ya awali.

“Tumefanya tafiti kuangalia maendeleo ya watoto hawa darasani na kubaini kuwa wana changamoto katika ujifunzaji na uelewa ukilinganisha na watoto wa akina mama ambao hawakugusana na viuatilifu,” amesema.

Mbali na matatizo ya ubongo na ujifunzaji, Dk Ngowi amesema tafiti hizo pia zimeonesha ongezeko la watoto wanaozaliwa njiti kwa wanawake wanaotumia au kugusana na viuatilifu mara kwa mara.

“Utafiti umeonesha wazi kuwa wanawake wanaogusana na viuatilifu wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujifungua watoto njiti ukilinganisha na wale wasiogusana navyo,” amesema.

Mtafiti huyo amesema matumizi makubwa ya viuatilifu nchini yanaendelea kuongezeka sambamba na ongezeko la madhara ya kiafya, hali inayochochewa na ushawishi wa soko na biashara ya pembejeo za kilimo.

Amesema pamoja na hofu inayojengwa kuwa uzalishaji hauwezekani bila viuatilifu, takwimu zinaonesha wakulima wengi nchini bado hawavitumii kwa kiwango kikubwa lakini wanaendelea kuzalisha chakula cha kutosha.

“Taarifa zinaonesha ni asilimia 27 tu ya wakulima wanaotumia viuatilifu kwa kiwango kikubwa. Wakulima wengi bado wanatumia mbinu za kawaida na nchi inaendelea kujitosheleza kwa chakula na hata kuuza nje,” amesema.

Dk Ngowi ameonya kuwa madhara ya viuatilifu hayaishii kwa wakulima pekee, bali yanaathiri jamii nzima kupitia chakula kinacholiwa na wananchi.

“Wakulima wanaweka sumu kwenye mazao na mwisho wa siku mazao hayo yanaliwa na wananchi wote. Hivyo athari hizi zinagusa afya ya Watanzania wote,” amesema.

Akielezea hatari ya kemikali hizo, amesema baadhi ya viuatilifu vinaingilia mfumo wa homoni mwilini na vinaweza kuhusishwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo amesema ushahidi wa kisayansi unaendelea kuonyesha madhara makubwa ya kemikali hatarishi kwa afya ya binadamu, mazingira na bioanuai.

“Matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu duniani husababisha maelfu ya vifo na majeraha kila mwaka, hali inayohitaji hatua za haraka za kisera na usimamizi madhubuti wa matumizi ya kemikali hizo.

“Hivyo, tunaamini kwamba kupitia mradi huu wa miaka mitatu tutaweza kusaidia wakulima wetu kuweza kuondokana na matumiza haya ya viuatilifu na hata kufanya mpango huu kuwa endelevu baada ya mradi kutamatika,” amesema.

Warsha hiyo imezindua mradi wa miaka mitatu unaotekelezwa Tanzania, Kenya na Ethiopia kwa lengo la kusaidia wakulima wadogo kuachana na matumizi ya viuatilifu hatarishi na kuhamia kwenye kilimo ikolojia na mbinu salama za uzalishaji.

Ofisa Programu Mkuu wa Agenda, Silvani Mng’anya amesema mradi huo utalenga zaidi wakulima wa mboga na pamba katika maeneo yatakayochaguliwa baada ya tathmini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *