
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu “haitarudi nyuma” huku kukiwa na ripoti juu ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano kati ya Tehran na Washington.
Mohammad Bagher Zolghadr amesisitiza katika ujumbe aliotuma kwa wananchi wa Iran siku ya Jumatatu kwamba hakutakuwa na kusalimu amri wala kurudi nyuma na kueleza kuwa: “Hili limedhihirishwa katika medani ya vita, uga wa kidiplomasia na wananchi wanaomiminika mitaani na muqawama wao imara dhidi ya adui.
Katika ujumbe wake huo kwa wananchi wa Iran, Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ametilia mkazo umuhimu wa umoja wa kitaifa ili kuzuia njama za maadui.
“Hivi sasa nchi inahitaji umoja na mshikamano kuliko wakati mwingine wowote ili kuzikatisha tamaa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel,” amesema Mohammad Bagher Zolghadr.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la amesema umoja na mshikamano ni “uwanja mwingine katika vita,” na kwamba “juhudi za pamoja za kuzuia matamshi na hatua zozote zenye lengo la kuvuruga umoja wa Iran zitaiongoza Iran pendwa kwenye ushindi wa mwisho, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Mohammad Bagher Zolghadr amebainisha haya huku mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, chini ya upatanishi wa Pakistan yakiendelea kwa kuzingatia mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya vipengele 14 kwa lengo la kufikia makubaliano ya kuhitimisha vita.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani yamejikita katika kukomesha uvamizi katika medani zote na kwamba, suala la lnyuklia au kuhusu usimamizi wa Mlango Bahari wa Hormuz hayatajadiliwa.
