
Babati. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Babati mkoani Manyara, imetoa zuio la muda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua zozote kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amri ya zuio hilo la upande mmoja (ex parte temporary prohibitory) limetolewa Jumatatu Mei 25, 2026 na Jaji Irvin Mugeta alipotoa uamuzi mdogo katika maombi ya kupatiwa kibali cha kufungua maombi ya kupata amri ya kukataza au zuio.
Maombi hayo namba 12812 ya 2026 yamefunguliwa na Katibu Mkuu wa Chadema pamoja na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho dhidi ya Msajili, kutokana na barua ya Msajili aliyokiandikia chama hicho Mei 7, 2026 ikikitaka chama hicho kijieleze.
Katika barua hiyo ambayo mahakama iliinukuu, Msajili alikiandikia Chadema barua yenye kichwa cha habari: Yah kuwasilisha maelezo kuhusu kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa katika shughuli za chama chenu (Chadema).
Majibu ya barua hiyo yalipaswa kuwasilishwa kwa Msajili kabla ya Mei 5, 2026 saa 9:30 alasiri na kwamba muda umekwisha, hivyo Msajili anaweza kuchukua hatua muda wowote. Hivyo Chadema ikaamua kutafuta utetezi wake mahakamani.
Jopo la mawakili Chadema
Jopo la mawakili watatu wakiongozwa na wakili Mpare Mpoki, Nyaronyo Kicheere na Hekima Mwasipu, waliomba mahakama itoe amri ya upande mmoja (ex parte orders), kutokana na udharura wa hatua zinazoweza kuchukuliwa na Msajili.
Maombi hayo yamewasilishwa na kiapo cha wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, ambao ni Ruth Mollel, Mary Joachim na Dk Azavel Lwaitama.
Kulingana na kiapo cha wadhamini hao, kuna dalili Msajili wa Vyama vya Siasa ameshafanya uamuzi wa kukipiga marufuku Chadema kufanya shughuli zozote za kisiasa kwa kusimamisha usajili wake au kukichukulia hatua nyingine.
Akitoa sababu za maombi hayo kwa niaba ya mawakili wenzake, wakili Mpoki alisema kama Msajili wa Vyama vya Siasa hatazuiwa, kuna uwezekano kwamba anaweza kusimamisha usajili wa Chadema au kutoza faini wakati wowote.
Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba mnamo au kabla ya Mei 16, 2026, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa alikwenda ITV na kufanyiwa mahojiano na kusisitiza kuwa Chadema kitapigwa marufuku kisipotoa maelezo ya kuridhisha.
Waombaji katika maombi hayo wanasema wanaamini kwa dhati kwamba Msajili amekuwa akitenda dhidi yao mara kwa mara kwa upendeleo na kwamba kwa kauli yake hiyo ITV inaonyesha tayari ameshafanya uamuzi wake dhidi ya Chadema.
Kwa mujibu wa Wakili Mpoki na kulingana na barua ya Msajili, ni kwamba Msajili ndiye mlalamikaji, atakuwa shahidi na mwamuzi katika shauri lake mwenyewe, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za haki asilia au Natural Justice.
Pia, wakili huyo alisema kuwa mahitaji katika barua ya Msajili hayakujumuisha Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema. Kwa hiyo, iwapo mahakama haitamuingilia na kumkataza kuendelea, mdhamini aliyesajiliwa atahukumiwa bila kusikilizwa.
Uamuzi wa Jaji
Katika uamuzi wake mdogo, Jaji alisema kutoa uamuzi wake katika hatua hiyo ni rahisi kwani ni kupima kama waombaji wameonyesha sababu tosha za kutaka kupewa nafuu waliyoiomba mahakamani kupitia maombi yao hayo.
Jaji Mugeta alisema amri ya muda ya kukataza inayotafutwa ni amri kwa asili na imewekewa vigezo vya kutimizwa kabla ya kutolewa kwa amri hiyo.
Moja ni kuwepo kwa shauri juu ya masuala ya ukweli unaodaiwa na pili kuonyesha umuhimu wa kuingilia kumlinda mdai kutokana na madhara yasiyorekebishika anayoweza kuyapata kabla haki yake ya kisheria haijathibitishwa na mahakama.
Msajili kuwa mlalamikaji na Jaji
Kigezo cha tatu ni kwenye mizani ya kupima madhara na mateso ambayo mwombaji atakayopata endapo amri inayoombwa isipotolewa.
Jaji Mugeta alisema Chadema ni chama cha siasa na kinajishughulisha na siasa na pia kinamiliki mali, huku Katibu Mkuu akishughulika na shughuli za kila siku na wadhamini wa chama wamekabidhiwa usimamizi wa mali za chama.
“Kwa kweli, kama ilivyowasilishwa zaidi na Wakili Mpoki, barua ya Msajili kutaka maelezo inashughulikiwa na Katibu Mkuu peke yake. Ikiwa Wadhamini Waliosajiliwa pia walipaswa kujumuishwa katika notisi hiyo ya Msajili, basi ni jambo la thamani linalopaswa kuzingatiwa na mahakama,” alisema Jaji.
“Zaidi ya hayo, Chadema inadai, kwa asili ya notisi ya mahitaji, Msajili ni mlalamikaji, shahidi aliyekusudiwa na hakimu kwa sababu yake mwenyewe.”
“Hakika, Msajili ameibua masuala hayo ambayo Chadema wanapaswa kuyatolea maelezo. Ikiwa ukweli huo humfanya Msajili asiye na upendeleo ni suala linaloweza kutatuliwa na mahakama kwa kusikiliza,” amesema.
“Inatosha kusema hivyo, masuala mawili yaliyotajwa hapo juu yanatosha kuhalalisha kushikilia kuwa kigezo cha kwanza kimefikiwa. Ninashikilia kuwa ombi linaonyesha kuwa linaweza kusikilizwa (triable) na mahakama,” alisisitiza Jaji.
Kuhusu kiwango cha hasara kinachoweza kupatikana ikiwa amri hiyo haitatolewa, Jaji Mugeta alisema ni msimamo wa sheria kuwa ni lazima hasara iwe kwa namna ambayo haiwezi kulipishwa kwa njia ya fidia.
“Nimejaribu kufikiria fidia ambayo Chadema inaweza kupata kwa hasara ambayo itatokana na shughuli za kisiasa kusimamishwa, lakini kwa kweli sioni,” alisema Jaji.
“Kwa maoni yangu, shughuli za kisiasa za vyama vya siasa lazima zishughulikiwe kwa uangalifu kwani zinaunda utawala wa nchi na michakato ya utekelezaji wa haki za kidemokrasia za raia,” alisema Jaji Mugeta katika uamuzi wake huo.
“Marufuku yoyote ya kisiasa kwa kusimamisha usajili zitasababisha hasara isiyoweza kurekebishwa kwa maana ya muda uliopotea kwa kushindwa kufanya shughuli za kisiasa katika kipindi cha kusimamishwa,” alisema Jaji na kuongeza kuwa:
“Pia itasababisha kupungua kwa nafasi kwa raia kushiriki siasa na ukosefu wa usimamizi wa mali za Chadema. Ninaelewa hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ni pamoja na faini.”
“Nakubali kutozwa faini kunaweza kulipwa kwa kurejesha fedha. Lakini kwa kuwa haiwezi kutabiriwa adhabu itakayotolewa endapo Msajili hatoridhika na maelezo ya Chadema, mizania ya haki kwa uzito mkubwa ipo kwa waombaji wa amri,” amesema.
“Kusimamishwa kunaweza kuwa chaguo pia. Hasara itakayopatikana kutokana na kusimamishwa itakuwa isiyoweza kupimika kiasi kwamba hakuna aina ya fidia inaweza kupunguza hasara,” alieleza Jaji Mugeta.
Achambua sababu za Msajili
Mwisho, Jaji alisema katika barua hiyo, Msajili ameeleza sababu za kwa nini achukue hatua za kusimamisha au kutoza faini, ikiwa ni pamoja na tabia ya Chadema kufanya kashfa, kejeli na kauli za uchochezi dhidi ya Serikali na viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jaji alisema katika hati ya kiapo, Chadema inakanusha madai hayo kwa kueleza kuwa chochote wanachofanya kinahusu kutekeleza haki na mamlaka kama chama cha siasa cha upinzani, na wanafanya hivyo kulingana na sheria za nchi.
“Katika hukumu yangu, kama kauli ni ya kipuuzi, kashfa au uchochezi inategemea hali ya kila kesi moja na mazingira pamoja na enzi katika historia ya nchi.”
“Kinyume chake, kusimamishwa kwa shughuli za chama cha siasa kunaweza kusababisha kutoweka kabisa kwa walioathirika, kwani wanachama wanaweza kukata tamaa na kujiunga na vyama vingine au kuamua kuishi bila kujiunga na chama chochote,” amesema.
“Kwa hivyo, kwa usawa wa urahisi, usajili wa Chadema ukisitishwa, itapata tabu zaidi, dhiki na hasara kutokana na kuzuiwa kwa amri inayoombwa kuliko itakavyokuwa kwa wajibu wa maombi kutokana na mwombaji kupewa amri,” alisema Jaji Mugeta.
Jaji alisema kutokana na aliyoyaeleza, hana shaka yoyote akilini kuwa hii ni kesi inayofaa kutoa maagizo ya muda ya marufuku kwa hatua zozote kuchukuliwa hadi maombi hayo ya kupatiwa kibali cha kufungua maombi ya zuio yatakaposikilizwa.
Kulingana na Jaji, kwa kuwa agizo lake hilo ni la muda na limetolewa baada ya kusikilizwa kwa upande mmoja, hakuna amri kwa upande wowote kulipa gharama za kesi.
