Fikiri apania heshima CoastalFikiri apania heshima Coastal

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema licha ya mwanzo wake mzuri na kikosi hicho tangu alipojiunga nacho, kwa sasa sio muda wa kuangalia suala la mkataba mpya, bali malengo ni kuona wanazidisha kiwango cha mapambano.

Kocha Fikiri alisema mkataba wake na timu hiyo unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu, japo suala la yeye kuongeza mwingine au kutafuta changamoto mpya, ni mapema kulizungumzia kwa sasa.

“Malengo yangu ya kwanza ni kuona timu inafanya vizuri na kutoka nafasi za kucheza ‘Play-Off’ ya kupigania kubaki Ligi Kuu Bara, ni kweli nimeanza vizuri kiasi lakini suala la mkataba mpya tuachane nalo kwa sasa,” alisema.

Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo tangu amekabidhiwa, Fikiri alisema hakuna mabadiliko makubwa ya kiuchezaji aliyofanya hadi sasa, isipokuwa alichofanya ni kutengeneza muunganiko mzuri kwa wachezaji wa kikosi hicho ili kuongeza ushindani.

Fikiri alifikia makubaliano ya kujiunga na kikosi hicho, akichukua nafasi ya Mohamed Muya aliyeondoka Aprili 8, 2026, kutokana na mwenendo mbaya, ambapo kocha huyo wa zamani wa KenGold ya jijini Mbeya, ameanza vyema maisha yake mapya.

Kocha huyo ameiongoza Coastal Union katika mechi saba za Ligi Kuu Bara hadi sasa, ambapo kati ya hizo ameshinda nne na kupoteza tatu, kikosi hicho kimefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10.

Pia, Fikiri ameiongoza Coastal katika mechi mbili za Kombe la Shirikisho la CRDB na kushinda zote, akianza kwa kuifunga Pamba Jiji mabao 2-0, hatua ya 16 bora, kisha robo fainali ikaichapa Singida Black Stars kwa penalti 4-2 baada ya suluhu ya (0-0) dakika 90.

Ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Singida, ukamfanya Fikiri kuipeleka timu hiyo hatua ya nusu fainali ambapo itakutana na Simba. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Juni 20, 2026.

Kocha huyo hakuwa timu baada ya kuachana na KenGold, Septemba 17, 2024, kutokana na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu, jambo lililosababisha kushuka daraja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *