
HESABU za kocha wa Azam FC, Florent Ibenge ni kukusanya alama nne kuanzia sasa akibakisha mechi tano za Ligi Kuu Bara kwani anaamini zinamtosha kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Ibenge hesabu zake zinakwenda vizuri kwani hivi sasa Azam yenye pointi 52, ikizipata hizo nne itafikisha 56 ambazo Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne pekee inaweza kuzifikia kwa zile zilizo chini.
Singida ili izifikie pointi 56, inapaswa kushinda mechi zote tano zilizobaki dhidi ya JKT Tanzania (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), Tanzania Prisons (nyumbani), Simba (ugenini) na Fountain Gate (ugenini).
Hata hivyo, pia itailazimu kufunga mabao mengi zaidi ikae juu ya Azam kwani hivi sasa imeachwa kwa tofauti ya mabao 22. Wakati Azam ikiwa nafasi ya tatu, kinara ni Yanag yenye pointi 60, ikifuatiwa na Simba iliyokusanya pointi 58.
Azam iliyocheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwa mara ya kwanza ikiwa chini ya Ibenge, kocha huyo Mkongomani alisema anapambania nafasi nyingine ya kurejea kimataifa.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Ibenge alisema mechi tano zilizosalia jambo la msingi ni kupata alama nne zitakazowaweka katika nafasi ya kushiriki michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
“Ikitokea tukashinda mechi zote litakuwa jambo muhimu zaidi, ila hesabu kali ni kupata pointi ambazo hazitafikiwa na timu zilizopo chini yetu,” alisema Ibenge na kuongeza;
“Wachezaji wanaandaliwa vizuri na wanapaswa kutambua kila mechi inahitaji morali ya juu na kuipambania timu ili kufikia malengo yake.”
Azam katika mechi hizo tano zilizobaki kwenye Ligi Kuu Bara itacheza dhidi ya Fountain Gate (ugenini), Mashujaa (nyumbani), Yanga (ugenini), Coastal Union (ugenini) na Dodoma Jiji (nyumbani).
